Habari Mseto

Nancy Macharia anashindwaje kujieleza kwa Kiswahili?

April 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA HENRY INDINDI

WIKI iliyopita Jumatano katika uangalizi wa mafunzo ya mfumo mpya wa elimu wa umilisi na utendaji (CBC), nilishuhudia kioja.

Viongozi mbalimbali katika wizara ya elimu walikuwa katika maeneo tofauti ya nchi wakishuhudia kuzinduliwa na kuangalia kuendelea kwa awamu nyingine ya mafunzo kwa walimu watakaokuwa nyanjani kutekeleza mfumo huu mpya wa elimu.

Niliguswa hasa na kisa kimoja cha Bi. Nancy Macharia anayesimamia Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) kushindwa kujieleza katika Kiswahili alihojiwa na mwanahabari Evans Asiba wa Citizen TV mjini Nakuru.

Ingawa mwanahabari huyu alimhoji au kuyauliza maswali yake katika Kiswahili chepesi na cha kawaida sana, mhojiwa ambaye ni nguzo muhimu na taswira muhimu katika elimu ya taifa letu hakuweza kabisa kuyajibu maswali aliyoulizwa katika Kiswahili. Yaani, aliyaelewa maswali lakini akahiari kuyajibu kwa kutumia lugha ya Kiingereza.

Hili lilinitaabisha sana kuhusu taswira ya Kiswahili na jinsi usimamizi wa taasisi na asasi mbalimbali za kielimu nchini humu unavyokitazama na kukichukulia Kiswahili kama lugha na somo.

Hivi wanafunzi wanaojua kwamba huyu ndiye msimamizi wa walimu na hawezi kujieleza katika Kiswahili hata kiwe cha kimsingi cha kujieleza, watalichukuliaje somo hilo darasani?

Ningemwelewa na kumwonea imani ikiwa si raia wa Kenya na ikiwa hasa hakusomea humu nchini. Hakuna yeyote anayeweza kudai kwamba maswali wanayouliza wanahabari wanapowahoji viongozi hawa huwahitaji wahojiwa kutumia Kiswahili fasaha sana kuyajibu.

Kwa hivyo, kiongozi wa walimu ambaye mienendo na kauli zake vinapaswa kuwa mfano wa kuigwa, anapoelewa Kiswahili asiweze kuzungumza ilhali ni lugha yake ya taifa, ninatia walakini katika jinsi uongozi wa asasi mbalimbali za taifa letu unavyokuwa.

Kusema la kweli, ni taswira ya kusikitisha kwa uongozi wa elimu kuwa hivyo katika taifa letu. Tunaelewa kwamba baadhi yao hawakupata nafasi ya kusoma Kiswahili shuleni kutokana na sera mbaya za elimu wakati huo, lakini hakuna yeyote katika hao aliyezuiwa kujituma kwenda na uchao katika utendakazi wa wizara na asasi wanazosimamia.

Kitu hakiwi na thamani isipokuwa kikitumikishwa na kuonewa fahari. Hili ndilo dogo ambalo mimi raia wa Kenya nitalitarajia katika raia wote wenzangu na hasa walio katika ngazi mbalimbali zinazoathiri jamii moja kwa moja.

Tunapaswa kufikia viwango vya kuwahoji watu kama hawa katika lugha ya Kiswahili ndipo tuwape nyadhifa mbalimbali za kusimamia.

Hatuna thamani ya taifa na utaifa na ndiyo sababu hatujali ikiwa lugha ya taifa ina thamani yoyote. Bi Nancy Macharia anawasimamia walimu wengi wakiwamo wanaofunza lugha ya Kiswahili.

Ikiwa ana walakini katika uzungumzaji wa Kiswahili akubali kuwa mwanafunzi wa kwanza wa mwalimu yeyote wa Kiswahili anayemsimamia ili tunapomwona tuione taswira kamili ya elimu na thamani ya elimu katika taifa hili.

Ninalitarajia lilo hilo kutoka kwa Waziri wa Elimu, Prof. George Magoha. Katika hotuba nyingi nyingi anazozitoa kuelekeza wizara ya elimu na taifa letu, itakuwa taswira ya kupendeza ikiwa naye atazitoa baadhi ya hotuba zake katika Kiswahili.

Tuheshimu na kuthamini taifa tunalohudumia. Heshima na thamani kwa taifa huanzia katika heshima na thamani katika vito vyake vikiongozwa na lugha ya taifa.