Habari Mseto

Nanok akemea ODM kumvua wadhifa

June 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY LUTTA

GAVANA wa Turkana Josphat Nanok amekashifu chama cha ODM kwa kumpokonya cheo chake cha naibu mwenyekiti wa kitaifa wa chama akisema kilikiuka katiba na kanuni zake.

Mnamo Alhamisi, Baraza Kuu la ODM (NEC) na maafisa wa chama hicho, waliamua kwa kauli moja kumvua wadhifa huo na kumpa Mbunge wa Loima, Jeremiah Lomorukai ambaye pia anatoka kaunti hiyo ya Turkana.

Uamuzi huo unajiri siku kadhaa baada ya Bw Nanok kutangaza wazi kwamba atamuunga mkono Naibu Rais William Ruto katika azma yake ya kuwa rais mwaka wa 2022.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Jumapili lakini yaliyofanyika Ijumaa, Gavana Nanok alisema hatua hiyo inakwenda kinyume na katiba ya chama hicho kinachoongozwa na Raila Odinga.

“Nashangaa kwamba ODM inakiuka katiba yake ili kudumisha ufuasi wake katika Kaunti ya Turkana. Hizi ni mbinu za zamani zilizotumiwa na Kanu katika miaka ya ’70 na ’90 ambazo hazina mashiko nyakati hizi,” alisema.

“Ikiwa ODM inadai inaheshimu demokrasia, inafaa kufuata utaratibu rasmi wa kuondoa afisa wake na kuchagua mwingine. Afisa anayeondolewa sharti aitwe na kupewa nafasi ya kujitetea,” alisema.

Kuwasilisha pendekezo

Aliongeza kuwa, NEC inapaswa kujadili suala hilo na kuwasilisha pendekezo la kuondolewa kwa afisa husika kwa Baraza Kuu la Uongozi (NGC).

Gavana Nanok alisema siasa inahusu masilahi ya wananchi ambao wako huru kuamua mwelekeo wao ikiwa wanahisi kutoridhika.

Alisema anakerwa na viongozi wa ODM, ambao alidai huwatumia watu wa jamii ya Turkana kama “vyombo vya kuwapa kura” kwa manufaa yao binafsi.

“Waturkana walipigia ODM kura kwa wingi wakati wa uchaguzi mkuu uliopita lakini wakatelekezwa na kusahauliwa baadaye,” Bw Nanok akasema.

Hata hivyo, alisema atasalia kuwa mwanachama wa ODM na kuendelea kuwatumikia watu wa Kaunti ya Turkana kama gavana wa ODM hadi muhula wake utakapokamilika mnamo 2022.