NASAHA ZA RAMADHANI: Tukague nafsi zetu msimu huu wa mfungo unapokaribia mwisho
KWA jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye Kurehemu.
Tuna kila sababu ya kumshukuru Allah (SWT) kutufikisha Ijumaa ya mwisho katika mwezi huu wa Ramadhani. Palipo uhai na uzima, Ijumaa ijayo hatutakuwa ndani ya kipindi hiki cha mfungo. Itakuwa labda siku ya pili au ya tatu baada ya Sikukuu ya Idd-Ul-Fitri.
Tumuombe Allah atufikishe, Insha’ Allah.
Ndugu msomaji, mada ya leo hasa ni kuangalia kama tulinufaika kivyovyote na kuja kwa mwezi huu wa Ramadhani.
Mwezi huu umekuwa kama mtu kupewa hundi au cheki na bilionea mkubwa na kuambiwa aandike kiwango cha pesa anachohitaji.
Chochote utakachoandika, atakupatia. Mwenyezi Mungu anasema, “Na waja wangu watakapokuuliza kunihusu, basi waambie hakika mimi nipo karibu. Najibu maombi ya mwombaji pindi anaponiomba…” (Al Baqara, 2:186).
Mwenyezi Mungu ametushauri kwamba tumuombe chochote tunachotaka wakati huu wa mwezi wa Ramadhani. Yeye yupo karibu nasi. Hii ni fursa iliyopo siku zote, lakini ndani ya Ramadhani, malipo huwa makubwa zaidi.
Kwa kuwa tupo ukingoni mwa mwezi huu, hapana budi ila kwa kila mmoja wetu kuitazama kwa makini hadithi hii ifuatayo.
Mmoja wa maswahaba wakubwa wa Mtume Muhammad (SAW) kwa jina Abu Hureirah (RA) alimnukuu akisema hivi kuhusu Ramadhani: “Umekujieni mwezi wa Ramadhani wenye Baraka. Allah ameamuru kwenu ni lazima kufunga katika mwezi huu. Katika mwezi huu inafungwa milango ya mbinguni na inafungwa milango ya motoni, na mashetani wanafungwa pia. Katika mwezi huu Allah ameandaa usiku ambao ni bora kuliko miezi elfu moja. Yule mwenye kuharamishiwa heri zake, hakika huyo ameharamishiwa heri nyingi sana.”
Je, ukiikagua nafsi yako, unadhani umenufaika na kuja kwa ibada ya Saum? Kama jibu ni la, unafanya juhudi gani kati ya leo na Jumanne?