Habari Mseto

National Bank benki ya kwanza kupata hasara ya mamilioni

August 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

BENKI ya National Bank imepata hasara ya Sh282.7 milioni katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo kufikia Juni 2018.

Katika kipindi kama hicho 2017, benki hiyo ilipata faida ya Sh179.8 milioni. Hasara hiyo ilisemekana kutokana na kupungua kwa kiwango cha riba na mapato yasiyotokana na riba.

Mapato kutokana na riba yalipungua kwa asilimia 9.6 kutoka Sh4.56 bilioni hadi Sh4.12 bilioni huku mapato yasiyotokana na riba yakiwa yamepungua kwa asilimia 13 hadi Sh1.1 bilioni.

Kutokana na hilo, mapato yalipungua kwa asilimia 10.1 hadi Sh3.66 bilioni nayo gharama ilipungua kwa asilimia 8.2 hadi Sh3.5 bilioni hasa kutokana na kupunguka kwa mikopo kwa asilimia 80 hadi Sh47.8 milioni.

Lakini benki zingine kama vile Kenya Commercial Bank na Cooperative zilipata faida kubwa.