Habari Mseto

Ndani maisha kwa kumuua mwenzake ili abaki akimumunya mapeni ya sponsa

November 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMKE raia wa Rwanda aliyemuua mwenzake wakipigania ‘sponsa’  Alhamisi alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

Jaji Jessie Lesiit alimsukumia kifungo hicho Bi Antoinette Uwineza baada ya kumpata na hatia ya kumuua mwanamke akiwa mja mzito.

Wote raia hao wa Rwanda walikuwa wanapigania mwanaume Mzungu aliyekuwa akiwaongoa kimapenzi.

Akipitisha hukumu, Jaji Jessie Lesiit alisema, Bi Antoinette Uwineza alifanya ukatili kumuua mama  akiwa na mimba.

Bi Uwineza alidaiwa alikuwa akimng’ang’ania mwanaume mmoja na marehemu, na kwamba alitekeleza mauaji hayo asalie na bwana huyo.

Lakini sasa mahakama ilisema hata naye atatenganishwa na ‘mume’ yule maisha.

“Hii mahakama imekupata na hatia ya kumuua Micheline Uwabwabiji katika hoteli moja jijini Nairobi mnamo 2012 akiwa na mimba,” Jaji Lesiit alisema akipitisha hukumu.

Jaji Lesiit alimweleza raia huyo wa kigeni kuwa katika Katiba ya na Sheria nyinginezo maisha ya binadamu uthaminiwa sana na hakuna “ tu hata mmoja amekubaliwa kumuua mwenzake.”

Jaji alisema maisha ya binadamu hutolewa kwa kila mja na Mwenyezi Mungu na anayeyachukua maisha ya mwingine lazima apambane na makali ya sheria.

Mahakama ilimweleza mshtakiwa kuwa chini ya sheria za nchi hii adhabu inayotolewa kwa wanaopatikana na hatia ni kunyongwa kwa kutiwa kitanzi ama kuadhibiwa kifungo cha maisha jela.

Jaji huyo alimweleza mshtakiwa ni jukumu la mahakama kuhakikisha kuwa maisha yanalindwa na wanaosababisha uhai wa mwingine kumtoka lazima waadhibiwe ipasavyo.

“Utahukumiwa kulingana na sheria za Kenya kwa vile ulitekeleza uhalifu huo ukiwa humu nchini,” Jaji Lesiit alimweleza mshtakiwa.

Aliongeza kumfafanulia kuwa mahakama iko na mamlaka ya kuchagua hukumu itakayopitisha dhidi ya mmoja, aidha anyongwe ama atumikie kifungo cha maisha gerezani, akumbane na mauti akiwa mle.

“Kulingana na ushauri uliotolewa na Mahakama ya Juu hivi karibuni kuhusu adhabu ya kifo, sasa majaji wako na mamlaka ya kuchagua adhabu watakayopitishwa dhidi ya mmoja,” Jaji Lesiit alimweleza mshtakiwa.

Wakili John Swaka aliyemtetea mshtakiwa aliomba mahakama imwonee huruma  raia huyo wa kigeni. Bw Swaka alisema mshtakiwa alikuwa ameachilliwa kwa dhamana na alifuata maagizo ya mahakama.

“Naomba hii mahakama imwonee huruma mshtakiwa ikipitiasha hukumu,” alisema Bw Swaka.

Upande wa mashtaka ulioongozwa na wakili Evalyn  Onunga alisema mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza chini ya sheria za nchini.

“Naiachia mahakama jukumu la kupitisha hukumu. Sina mengine ya kueleza,” alisema Bi Onuga.

Bi Uniweza mwenye umri wa miaka 31 alikabiliwa na shtaka la kumuua Uwabwabiji katika hoteli  ya Bahara iliyo katika eneo la River Road 2012.

Jaji Lesiit alisema upande wa mashtaka ulithibitisha Antoinette alimuua mwenzake waliyekuwa wanang’ang’ania mshikaji mmoja raia wa Uingereza.

Bi Uwineza alikuwa ameshtakiwa pamoja na  Alexander Kiole Mutie na Kassim Oyamo Odiwuor almaarufu Odi walioachiliwa baada ya kukosekana ushahidi wa kuwezesha korti kuwaadhibu.

Odi na Mutie walihusishwa na mauaji hayo kwa kupatikana na simu ya marehemu. Mutie alimweleza Jaji Lesiit aliuziwa simu hiyo na Odi aliyesema akijitetea kuwa aliinunua kutoka kwa jamaa.

Mahakama iliwaachilia kwa kutousika na mauaji hayo.

Marehemu alikutwa ameuliwa ndani ya lojing mtaa wa River Road Nairobi. Alivishwa mfuko wa nailoni kichwani baada ya kunyongwa.

Bw Swaka atakata rufaa.