Habari Mseto

Ndani siku 14 kwa kuua mkewe Leba Dei

May 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

MAUREEN KAKAH na DANIEL OGETTA

Mwanaume aliyemuua mkewe mjamzito Pangani, Kaunti ya Nairobi hapo Leba Dei atasalia korokoroni kwa kipindi cha wiki mbili.

Hakimu mkuu wa mahakama ya Makadara, Bw Heston Nyaga aliamuru Mohamed Abdullahi Abdi kusalia korokoroni kwa siku 14 ili kuwaruhusu polisi kukamilisha uchunguzi wa mauaji hayo.

“Mshukiwa asalie korokoroni hadi Mei 16,” alisema hakimu Nyaga.

Polisi walieleza korti kwamba walihitaji muda zaidi wa kufanya upasuaji, kuandaa ripoti za uchunguzi wa matibabu na vilevile kuandaa rekodi za shahidi.

Mnamo Jumanne Aprili 30, inadaiwa mshukiwa alimpiga na kumjeruhi mwendazake ambaye alivuja damu hadi akafa Mei 1.

Katika juhudi za kuokoa maisha yake, mwendazake alikimbizwa Hospitali ya Pumwani lakini kwa bahati mbaya, akakata roho alipokuwa anahamishwa hadi Hospitali kuu ya Kenyatta kwani alikuwa katika hali mahututi.

Mshukiwa alikamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Pangani mida ya mbili usiku wa tukio hilo.

“Muda wa kuandaa uchunguzi haukutosha kutokana na hali ya mauaji haya hivyo basi tunaomba mshukiwa azidi kukaa rumande kwa siku kumi na nne zaidi ili tuweze kuandaa ripoti kamili ya uchunguzi wetu,” Inspekta Franklin Adu alisema.