Ndovu waliotoroka mbugani wasababisha kifo cha mwanamume mmoja Timboroa
Na PETER MBURU
MWANAMUME wa umri wa miaka 65 aliaga dunia Alhamisi eneo la Timboroa, Kaunti ya Baringo huku mwingine mwenye umri wa miaka 19 akijeruhiwa, baada ya kupigwa risasi wakati maafisa wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS) walikuwa wakiwarejesha mbugani ndovu watano ambao walikuwa wametoroka.
Bw Julius Mwenda Kihara alifariki alipokuwa akiwahiwa katika hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Moi (MTRH) kutibiwa, baada ya kupigwa risasi.
Bw Kihara alikuwa amepewa huduma ya kwanza katika kituo cha afya cha Timboroa kabla ya kutumwa MTRH kwa matibabu zaidi, lakini akathibitishwa kufa alipowasili hospitalini.
Bw Emmanuel Kipchumba mwenye umri wa miaka 19 naye alijeruhiwa asubuhi na ndovu hao katika Ziwa Timboroa, wakati tu ndovu hao walifika maeneo wanapoishi wakazi.
Alitibiwa katika kituo cha afya cha Timboroa, kisha akatumwa katika hospitali ya Kaunti Ndogo ya Eldama Ravine ambapo anazidi kupokea matibabu.
Ndovu hao walitoroka kutoka msitu wa Timboroa saa za asubuhi, wakavuka barabara kuu ya Nairobi-Eldoret na kuelekea maeneo wanapoishi watu karibu na mtaa wa Shauri, kabla ya shirika la KWS kufahamishwa.
Washtuka
Wakazi walikumbwa na mshtuko kufuatia visa hivyo, wakisema hawajawahi kushuhudia visa vya wanyamapori, hasa ndovu, kufika eneo hilo.
“Hii ni mara ya kwanza kwani tumekuwa tukifanya kilimo huko ndani yam situ lakini hatujawahi kuwaona Wanyama hawa. Eneo hili huwa hakuna Ndovu, Simba ama Wanyama wengine wa aina hiyo,” akasema Bi Grace Wanjiku, mkazi wa eneo hilo.
KWS Ijumaa ilisema ndovu hao walipotea njia walipokuwa wakisafiri kutoka Laikipia kuelekea Mau, ikiwarai wakazi kuwa makini.
“Kundi la ndovu watano wa kiume waliokuwa wakihama kutoka Laikipia kuelekea Mau walipotea njia na wanazunguka karibu na msitu wa Timboroa. Timu zetu zimefika eneo hilo na yeyote aliye eneo hilo anashauriwa kuwa makini,” KWS ikasema kupitia ujumbe.