Habari Mseto

NEMA yafunga viwanda vitatu

April 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA COLLINS OMULO

MAMLAKA ya Kitaifa ya Mazingira Nchini(NEMA), Jumatano ilifunga viwanda vitatu eneo la Nairobi Kusini kwa kutoa gesi hatari kwa afya ya binadamu wakati wa oparesheni zake.

Viwanda hivyo Powerex, Edible Oils na Usafi Plus, vinapatikana kando ya barabara ya Nairobi kuelekea Mombasa.

Mamlaka hiyo kisha ilitwika serikali ya kaunti ya Nairobi jukumu la kufanya uchunguzi kuhakikisha viwanda hivyo vinazingatia sheria kabla ya kufunguliwa.

Waziri wa Mazingira, Bw Keriako Tobiko, wiki jana aliagiza uchunguzi ufanyiwe kwa baadhi ya viwanda vinavyotoa gesi hatari nyakati za usiku ili vifungwe endapo vitapatikana na hatia.

“Ndiyo viwanda hivyo vitatu vimefungwa kwa muda usiojulikana ili kutoa nafasi ya uchunguzi. Tutahakikisha vinatii sheria kabla havijarejelea shughuli za utengenezaji bidhaa,” akasema Bw Tobiko jana.

Wiki mbili zilizopita, serikali ya kaunti ilikuwa imeonya kwamba viwanda 20 vilivyoko katika eneo la Nairobi Kusini vingefungwa na wamilki wake kushtakiwa mahakamani ikiwa vingeendelea kuchafua mazingira.

Waziri wa Mazingira wa kaunti, BW David Makori, alikuwa amesema kuna viwanda viwili ambavyo vilikuwa vimetajwa sana na wenyeji kama vinavyoshukiwa kutoa gesi hatari nyakati za usiku.

Mamlaka hiyo ya NEMA imeendeleza juhudi zake dhidi ya wanaochafua mazingira, wakati ambapo pia imeweka mikakati ya kuhakikisha marufuku ya mifuko ya plastiki inazingatiwa.

Katika juhudi hizo, NEMA pia imepinga mifuko ambayo ilianza kutumika baada ya mafuruku hiyo, ikisema kuwa ubora wa baadhi ya mifuko hiyo inayoagizwa nchini, ni wa chini mno.