Habari Mseto

NEMA yatisha kufunga chuo kikuu kwa kuchafua mazingira

June 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAMLAKA ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) imetisha kufunga chuo kikuu kimoja na kichinjio kaunti ya Kajiado kwa kukiuka sheria za kimazingira.

Maafisa kutoka makao makuu ya mamlaka hiyo wamekuwa wakizunguka katika kaunti hiyo ndani ya muda wa wiki moja kuhakikisha kuwa sheria za kutunza mazingira zinazingatiwa.

Mnamo Jumatano, Juni 19, 2024 maafisa hao walifika katika Chuo Kikuu cha Umma ambako walikagua miundo msingi ya kuondoa maji machafu na majitaka.

Watu wanaoishi karibu na chuo hicho wamelalamika kuwa maji machafu yenye uvundo humwagwa sehemu za wazi kando ya chuo hicho.

Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Ulinzi katika NEMA, Salome Machua alilaumu chuo hicho kwa kupuuza agizo lake la awali kwamba lirekebishe hitilafu hiyo kwenye miundo msingi yake ya kutoa maji machafu.

“Muundo msingi huu unatoa maji machafu katika maeneo ya karibu chuo kikuu cha Umma licha ya onyo kutoka kwa Nema. Huenda tukalazimika kukifungulia mashtaka chuo hichi au tuamuru kufungwa hadi kizingatie sheria,” akasema.

Bi Machua aliongeza hivi: “Tunalenga zaidi utupaji taka na maji-taka katika shule, mitaa ya makazi na vichinjio katika kaunti ya Kajiado.

Afisa Mkuu wa Idara ya Masuala ya Kifedha katika chuo hicho Abdi Swalah ambaye aliwapokea maafisa kutoka kwa Nema alikuwa na wakati mgumu kuelezea sababu ya chuo hicho kufeli kurekebisha miundomsingi ya kutoa maji-taka.