• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 3:13 PM
Serikali yapiga marufuku mikutano ya kisiasa Uhuru Park katika hatua ya kihistoria

Serikali yapiga marufuku mikutano ya kisiasa Uhuru Park katika hatua ya kihistoria

Na COLLINS OMULO

SERIKALI sasa haitaruhusu mikutano yoyote ya kisiasa kuandaliwa ndani ya bustani ya Uhuru na Central Park iliyokarabatiwa.

Onyo hilo lilitolewa na Waziri wa Ulinzi, Aden Duale Jumatano alipofika mbele ya kamati ya Seneti.

Waziri huyo alisema maeneo hayo mawili, ambayo ukarabati wayo umegharimu Sh1.18 bilioni, hayatatumika kuandaa mikutano yoyote kama vile ya kisiasa.

Mbali na hayo, aliwataka wanasiasa kutafuta ukumbi mwingine wa kufanyia mikutano yao, akisema bustani hizo ni mali ya wananchi.

“Hatutawaruhusu wanasiasa kuandaa mikutano yao ya kisiasa katika bustani hizo. Mpeleke mikutano yenu ya kisiasa kwingine. Wanasiasa watalazimika kutafuta ukumbi mwingine,” alisema CS Duale.

Waziri huyo alikuwa akijibu swali la Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kuhusu sababu ya kubomolewa kwa jumba maarufu la Uhuru Park Pavilion ambapo wanasiasa walikuwa wakiendesha mikutano.

“Kulikuwa na mantiki gani ya kubomoa eneo ambalo tulikuwa tulitumia kuhutubia wafuasi wetu?” aliuliza Bw Sifuna.

Wakati uo huo, Bw Duale alisema Alhamisi watakabidhi bustani hizo mbili kwa serikali ya Kaunti ya Nairobi pamoja na kutia saini mkataba wa maelewano (MoU) kati ya wizara yake na serikali ya kaunti kuhusu usimamizi wake katika kipindi cha mpito.

Alisema wanakaribia kumaliza ukarabati wa bustani hizo uliyoanza 2022 na ulikuwa ukifanywa na Jeshi la Ulinzi la Kenya.

“Ni asilimia 8 pekee ya kazi imesalia ikiwa ni pamoja na kuunganisha kisima kilichochimbwa katika Hifadhi ya Kati hadi tanki la maji na ujenzi wa bomba kuu ambalo limecheleweshwa kutokana na kazi zinazoendelea za KeNHA kwenye Barabara Kuu ya Uhuru,” Waziri alisema.

“Ili kuhakikisha tunamsaidia gavana, tumekubaliana tutaiacha nyuma timu yetu ya ufundi ikiwa ni pamoja na wahandisi na wasanifu majengo, kutia MoU ya kufanya kazi kwa kipindi cha miezi 6 ili kukamilisha zoezi hilo,” akaongeza Waziri Duale.

  • Tags

You can share this post!

Kuolewa kulinisaidia kutoroka mauti msituni Shakahola

Duale, Sakaja wavutania matumizi ya bustani za Central na...

T L