Ni rahisi kwa wafisadi kuhalalisha mali ya wizi Kenya – Ripoti
Na VALENTINE OBARA
SERIKALI ya Amerika imetilia shaka uwezo wa Kenya kurudisha mali zote za umma zilizoibwa.
Uchunguzi uliofanywa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni katika Serikali ya Amerika, ulionyesha kuwa ni rahisi mno kwa wahusika wa ufisadi hapa Kenya kuhalalisha mali zao za wizi kabla mkono wa sheria uwapate.
“Sheria zinahitaji kwamba polisi lazima wapate agizo la mahakama na watoe ushahidi unaothibitisha mapato ya washukiwa yalitokana na ufisadi, ndipo waruhusiwe kuitisha rekodi za kifedha za washukiwa kutoka kwa benki au kutwaa akaunti husika.
“Huwa hakuna usiri mkubwa katika utekelezaji wa hatua hii na hivyo basi wenye akaunti hizo wanaweza kufahamu mapema kuhusu mpango uliopo hivyo na watahamisha mali zao kwingine,” ikasema ripoti ya uchunguzi huo iliyotolewa wikendi.
Ripoti hiyo ilizungumzia pia mali inayopatikana kupitia njia nyingine za kihalifu kama vile ulanguzi wa dawa za kulevya, uwindaji haramu, biashara za bidhaa ghushi na hata ugaidi.
Huduma za kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu pia zilitajwa kama njia rahisi ya wahalifu hao kuhalalisha fedha zao, kwani hakuna sheria thabiti zinazowazuia kufanya hivyo.
Ripoti hiyo ilitolewa siku chache baada ya kufichuka kuwa familia ya Ngirita, ambayo imehusishwa pakubwa na wizi wa pesa katika shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), ilifanikiwa ‘kusafisha’ kiwango kikubwa cha fedha kabla uamuzi wa kuwashtaki kutolewa.
“Ingawa Kenya imepiga hatua katika utekelezaji wa mwongozo wa kuzuia uhalalishaji wa pesa haramu, bado kuna changamoto kuhusu utekelezaji kamili. Kenya inafaa ijitolee zaidi katika uongozi bora, juhudi za kupambana na ufisadi na kuboresha sheria zote zinazohusu uhalalishaji wa pesa haramu,” ripoti ya Amerika ikasema.
Ripotin hiyo imependekeza raslimali zaidi zitengewe asasi zinazohusika kupambana na ufisadi, hasa idara ya polisi ili kuboresha uwezo wa maafisa kufanya upelelezi kuhusu masuala mazito ya kifedha kwa njia huru.
Kenya inakabiliwa na janga la ufisadi hasa kutokana na wahusika kukosa kuadhibiwa.