Habari Mseto

Vijana wahimizwa kutumia teknolojia kuvuna pesa

May 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA LAWRENCE ONGARO

VIJANA wamehimizwa kukumbatia masuala ya kidijitali ili kuboresha maisha yao.

Waziri wa Teknolojia ya Habari (ICT) na Uchumi wa Kidijitali Bw Eliud Owalo alizuru Kaunti Ndogo ya Ruiru mnamo Jumatatu ili kujionea kituo kipya cha ICT katika wadi ya Biashara mjini Ruiru.

Waziri huyo aliandamana na Mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ara, diwani (MCA) na maafisa wa serikali.

Kituo hicho kina takriban kompyuta 104 na kimevutia vijana waliojitolea kuelewa jinsi ya kufanya kazi kidijitali na kupata pesa.

“Ninawahimiza vijana kujitokeza kwa wingi kuona ya kwamba wanajiunga na kituo hiki kwa manufaa yao wenyewe,” alisema waziri Owalo.

Bw Owalo alisema katika ulimwengu wa sasa, teknolojia ya ICT ndio inayowapa vijana ajira na kwa hivyo akawashauri wajitume.

Mwongozo wa mpango wa kujifunza ICT ulikuwa Jitume.

Alisema serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto imejitolea kuona ya kwamba Wizara ya ICT inawapa vijana nafasi ya kujitafutia ajira katika nchi za ng’ambo bila kusafiri hadi huko.

“Siku hizo iwapo una ujuzi wa kutumia vifaa vya kiteknolojia, bila shaka utapata nafasi tele za ajira katika nchi za ng’ambo,” alifafanua waziri huyo.

Alisema serikali ina mipango ya kuweka vifaa vya ICT katika masoko 25 kote nchini ambapo mama mboga atakuwa na nafasi bora ya kuuza bidha zake hata kwa mteja aliye mbali ambaye ataagiza na kupelekewa.

Vijana wakiwa kwa kituo cha ICT katika wadi ya Biashara. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Alieleza kuwa hivi karibuni, vifaa 1,450 vya ICT vitasambazwa kila sehemu nchini ili kuwapa wananchi nafasi ya kuendesha shughuli zao.

Naye Bw King’ara aliomba waziri kuhakikisha vifaa vya ICT vinasambazwa katika wadi nane katika eneobunge lake.

“Waziri mimi ningeomba ufanye juhudi kuona ya kwamba Ruiru kwa ujumla inasambaziwa vifaa vya ICT ili watu wangu wafaidike,” alisema mbunge huyo.

Bw King’ara aliwashauri vijana wajiepushe na mambo maovu kama unywaji wa pombe haramu na dawa za kulevya na badala yake wajifunze maswala ya ICT.

Mwakilishi wa wadi ya Kahawa Sukari Bw Kenneth Odhiambo, alitoa ombi eneo lake pia lipewe kipaumbele ili vijana waweze kunufaika na mpango huo.

“Waziri nakuomba ufanye juhudi ukiweza upitie eneo hilo ili ujionee mwenyewe. Kwa hakika, vijana wangu wanahitaji masomo hayo,” alisema Bw Odhiambo.

Mkufunzi mkuu katika kituo hicho Bw Stephen Ochieng’, aliwataka vijana popote walipo wajitume ili waweze kupata ajira ya haraka kupitia ICT.

Alisema iwapo mtu atajituma vyema, anaweza hata kuchota Dola 700 (sawa na Sh 89,670) kwa mwezi.

“Mimi ningependa kuwahimiza vijana wajitume mara moja ili waweze kuona matunda ya kazi yao,” alishauri Bw Ochieng’.