Habari Mseto

NiE: Base Titanium kufadhili shule 21 magazeti ya Taifa Leo

September 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na FARHIYA HUSSEIN

SHULE 21 kutoka Kaunti ya Kwale zitanufaika kupitia mradi wa Newspapers in Education (NiE) unaolenga kunoa wanafunzi masomoni.

Hii ni baada ya Kampuni ya Base Titanium kuahidi kununua nakala 2,700 za gazeti la Taifa Leo linalochapishwa na kampuni ya Nation Media Group kwa gharama ya Sh150,000 ambazo wanafunzi watatumia kujitayarisha kwa mtihani wao.

Akizungumza katika shule ya msingi ya Gazi kata ndogo ya Mswambweni, afisa wa uhamasishaji wa jamii, Mwanaidi Ali alisema mradi huo utawafaidi sana wanafunzi na kuinua viwango vya elimu.

“Viwango vya elimu katika kaunti hii vilikuwa vimeteremka sana. Lakini kupitia majaribio ya mitihani inayochapishwa katika gazeti la Taifa Leo wanafunzi wetu wataweza kusonga mbele,” alisema Bi Ali.

Aliongeza kuwa walianzisha mradi huo kwa kuwazawidi wanafunzi kadhaa.

“Tunatarajia mradi huu kuendelea mbele na kuhusisha hata kata ndogo ya Likoni. Magazeti yatakuwa yakigawanywa kila wiki huku shule moja ikipokea nakala 150,” alisema Bi Ali.

Gazeti la Taifa Leo huchapisha mitihani ya majaribio Jumatatu na Jumanne ambayo ni maswali ya shule ya msingi kisha Jumatano inachapisha majibu ya maswali hayo, huku Alhamisi na Ijumaa maswali ya mtihani wa kidato cha nne yakichapishwa. Majibu huwa Jumamosi.

Kila mwezi mada moja ya Insha huchapishwa katika gazeti hilo na mwanafunzi ambaye huongoza wengine kwa kuandika Insha bora huzawadiwa pamoja na shule na mwalimu wake wa somo la Kiswahili.

Msimamizi wa uimarishaji vipawa katika kampuni ya Base Titanium, Juma Omari, alisema wanajaribu kila wawezalo kuwasaidia wanafunzi wa shule ya msingi, upili na pia vyuo vikuu.

“Tuliona ni bora kuwanunulia hawa wanafunzi nakala za gazeti ili waboreshe somo lao la Kiswahili. Mradi huu tunatarajia utawafaidi wanafunzi wa Kwale na kata ndogo ya Likoni,” alisema Bw Omari.

Wanafunzi hao walizawidiwa shati tao pamoja na kalamu kwa majibu waliyotoa sahihi walipoulizwa maswali.

Wakati huo huo, Mratibu wa NiE, Bw Nuhu Bakari alisema kuwa lengo la mradi huo ni kuhamasisha na kuwapa moyo watoto na wanafunzi wengineo.

“Tatizo kubwa lilioko ni wanakipuuza Kiswahili. Hii imewafanya kuanguka mtihani mara kwa mara,” akasema Bw Bakari.

Aliongezea kuwa, kupitia nakala za gazeti la Taifa Leo wanafunzi wataweza kujiinua kielimu.

Aidha, aliwarai wanafunzi hao kujitolea vilivyo na kuhakikisha wanapitia nakala hizo.

Wanafunzi zaidi ya 2000 wamefaidika kupitia shirika a Base Titanium.

Pia, imeweza kusaidia jamii kwa ujumla kwa kuimarisha usafiri, chakula, kazi, afya na pia elimu.