Habari MsetoSiasa

Nilibandikwa jina 'Sultan' na maadui wangu, Joho afichua

September 26th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na WINNIE ATIENO

GAVANA wa Mombasa Ali Hassan Joho Jumatano alifichua kuwa alibandikwa jina ‘Sultan’ na mahasidi wake wa kisiasa ambao walilenga kumchafulia jina.

Akihutubu kwenye halfa ya kutathmini namna ugatuzi umeboresha hali ya maisha ya wakazi tangu 2013, gavana huyo aliwapongeza wakazi kwa kusimama kidete na yeye kwenye misukosuko yake ya kisiasa.

“Mahasidi wangu walinipachika majina hususan sultan ili kunitenganisha na wakazi. Sijawahi kujiita sultan na badala ya kuniharibia sifa, wakazi walilipenda,” akasema.

Alisema mahasidi wake wa kisiasa walifanya vikao na waandishi na kuwaonya wakazi dhidi ya kumchagua ‘sultan’ ambaye ataongoza kifalme.

Gavana huyo alisema masaibu yake yaliisha baada ya kinara wa ODM Raila Odinga ‘kusalimiana’ na Rais Uhuru Kenyatta.

Alifichua tangu ushirikiano huo uanze, urafiki wake na Rais Kenyatta umeimarika akisema huwa wanazungumza mara kwa mara.

Bw Joho ambaye alikuwa mpinzani mkali wa Bw Kenyatta alisema siku hizi yeye na Rais ni marafiki wakubwa akiwatangazia wakazi wa Mombasa kuwa vita vyake na kiongozi wa taifa vimekwisha.

Alisema maelewano kati ya kiongozi wa chama chake Raila Odinga na Bw Kenyatta yatafaidi wakenya pakubwa.

Wakati huo huo, Bw Joho alitoa wito kwa serikali kuu kuimarisha ugatuzi kwa kuwapa magavana nusu ya rasmilimali.