Nimekubali kifo cha Fidel, asema Ida Odinga akiadhimisha miaka tisa tangu afariki
NA FRIDAH OKACHI
MKE wa Waziri Mkuu wa zamani, Bi Ida Odinga amekiri kuishi na uchungu mwingi wa kumpoteza kifungua mimba wake Fidel Odinga miaka tisa iliyopita.
Akiandika kwenye mtandao wa Facebook, Ida alisema pengo lililoachwa na mwanawe haliwezi chukuliwa na mtu mwingine, akieleza kuwa hali hiyo imekuwa ikimsumbua kila siku ila amelazimika kukubali uhalisia wa mambo.
“Miaka imekimbia haraka sana tangu ulipoondoka. Leo ni miaka 9! Haraka ya ajabu! Lakini ilikuwa daima wewe, mwanangu Fidel Castro Makarios Odhiambo Odinga. Tangu siku ya kwanza nilipokubeba, hadi miezi mingi niliyokupakata kama mtoto mchanga, ulitaka kujitengemea, ili utulinde,” aliandika Bi Odinga.
Katika ujumbe huo alioupakia mitandaoni, alimmiminia sifa jinsi alikuwa mwana aliye na upendo, furaha na mkarimu.
Alionyesha kukubali hali hiyo kwa kuweka jitihada za kujifunza matukio yalivyo.
“Labda uliishi vya kutosha kwa sababu uliishi sawa. Kufariki kwako, bila shaka, kulinitikisa na kututikisa. Hakuna chochote katika ulimwengu huu, kitakachoweza kuchukua nafasi ya uwepo wako karibu nasi. Lakini katika miaka 9, tunatambua kwamba katika miaka 41 ya maisha yako, ulituandikia kumbukumbu nyingi za ajabu…Pumzika kwa amani, Fidel Obange wuod Nyagem.”
Fide Castro Odinga ambaye alikuwa mtoto wa kiume wa kwanza kwa familia ya Raila Odinga aliaga dunia Jumapili, Januari 4, 2015.
Alifariki baada ya kutoka kwenye sherehe usiku huo na kupatwa na maumivu akiwa nyumbani kwake huko Karen.