Nimetubu ‘dhambi’ na kuokoka, Gavana wa Kericho Eric Mutai sasa atangaza baada ya kuponea kutimuliwa
GAVANA wa Kericho Eric Mutai amesema kuwa ametubu “dhambi” zake na kuokoka na siku hizi anamfanyia Yesu kazi sambamba na kuwahudumia wakazi wa kaunti hiyo.
Akiongea Jumapili, Novemba 24, 2024 katika ibada eneo la Kipsitet, eneo bunge la Sigowet/Soin, Dkt Mutai alisema kuwa “siku hizi sina maneno mengi”.
Ibada hiyo ya shukrani iliandaliwa na makanisa mbalimbali katika kaunti ya Kericho na kuhudhuriwa na Rais William Ruto.
“Siku hizi nimetubu na kuokoka na ninamfanyia Yesu kazi. Kwa hivyo, ningependa kutangaza tena hapa kwamba nimeacha maneno mengi,” akasema kabla ya kumwalika rais ahutubie waumini.
Dkt Mutai alionekana kurejelea masaibu yaliyompata Oktoba 3, 2024 madiwani wa Kericho walipopitisha hoja ya kumtimua afisini.
Hata hivyo, gavana huyo alinusurika mnamo Oktoba 14, 2024 Seneti ilipobatilisha kutimuliwa kwake ni madiwani 31 pekee waliounga mkono hoja hiyo badala ya idadi hitaji kisheria la madiwani 32.
Kaunti ya Kericho iko na jumla ya madiwani 47 na hivyo hoja ya kumtimua Gavana Mutai ilihitaji kupata uungwaji mkono kutoka angalau thuluthi mbili ya madiwani hao ambayo ni sawa na madiwani 31.
Hii ni kwa mujibu wa hitaji lililoko katika Sehemu 33 (3) ya Sheria ya Serikali za Kaunti iliyopitishwa 2012.
Maseneta wengi walikubaliana na pingamizi iliyoibuliwa na wakili wa Gavana Mutai, Katwa Kigen, mteja wake alitimuliwa kwa njia haramu kwa hoja hiyo haikuungwa mkono na idadi hitajika ya madiwani.
Miongoni mwa tuhuma dhidi ya gavana huyo ilikuwa ukiukaji sheria wakati wa kuajiru wafanyakazi na kufuta wengine kiholela, matumizi mabaya ya mamlaka ya afisi yake, ukiuja wa Katiba, sheria kuhusu maadili na uongozwa miongoni wa zingine.
Madiwani 16, ambao ni wandani wa Dkt Mutai, walisusia upigaji kura kwa hoja hiyo iliyodhaminiwa na diwani wa Sigowet Kiprotich Rogony.