Nipeni muda tu nitabadilisha KBC, asema Nguna
MKURUGENZI Mkuu mpya wa Shirika la Kitaifa la Habari (KBC), Bi Agnes Kalekye Nguna, ameahidi kubadilisha sura ya shirika hilo la umma.
Akizungumza kwenye hafla ndogo ya kukabidhwa afisi yake mpya kufuatia uteuzi wake Ijumaa iliyopita, Bi Nguna ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Nchini (MOA), alikiri kuwa na kibarua kigumu mbele yake.
“Nimepokea uteuzi huu kwa moyo mkunjufu. Nina matumaini makubwa ya kubadilisha mambo. Nipeni muda, angalau nipate picha ya utendaji wa shirika. Nafikiri huko mbeleni nitaweza kuzungumzia kwa undani mpango niliyo nayo kubadilisha KBC,” alisema Bi Nguna.
Uteuzi wake ulifanywa na Waziri wa Teknolojia, Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Kidijitali, Bw Eliud Owalo. Wadhifa huo ulisalia wazi Desemba 19, 2024 baada ya Waziri Owalo kumtimua Bw Samuel Maina aliyekuwa anaushikilia kwa muda.
Uteuzi wa Bi Nguna unajiri mwezi mmoja baada ya Rais William Ruto kumteua aliyekuwa Mhariri Mkuu wa Shirika la Habari la Nation Media Group (NMG), Tom Mshindi kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakurugenzi wa KBC mnamo Janauri mwaka huu.