Habari Mseto

Nipewe mwili wa mume wangu nizike – Sarah Cohen

September 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na FATUMA BUGU

MZOZO umeibuka baina ya Bi Sarah Wairimu aliyekuwa mkewe bwanyenye Tob Cohen, na dadaye Gabriele Cohen kuhusu anayestahili kusimamia mazishi yake.

Jumatano, Bi Wairimu aliwasilisha ombi kwa hifadhi ya maiti ya Chiromo kutaka kukabidhiwa mwili kwa minajili ya mazishi ilhali jamaa za Cohen walitaka kumzika marehemu haraka iwezekanavyo kwa msingi wa imani za Wayahudi.

Kupitia kwa wakili wake Philip Murgor, Wairimu alitaka usimamizi wa Chiromo kutompokeza dadake Cohen mwili huo akidai kuwa Bi Wairimu angali mke halali wa Cohen.

Pia alidai kuwa Gabriele ndiye anayefaa kutafuta idhini kutoka kortini ya kumzika kakake na wala si Bi Wairimu inavyosemekana kwa sasa.

Haya yalijiri wakati upasuaji wa mwili wa marehemu ulikuwa ukiendelea Chiromo kutathmini kilichosababisha kifo cha Cohen.

Mnamo Jumanne, upasuaji huo uliahirishwa ghafla baada ya Bi Wairimu kupinga mwanapatholojia Dkt Peter Ndegwa kushiriki katika upasuaji huo akidai kwamba alikuwa na uhusiano wa karibu na maafisa wa idara ya upelelezi na hivyo angehitilafiana na matokeo ya upasuaji.

Bi Wairimu aliomba mahakama kumpa fursa ya kushuhudia upasuaji huo, ombi ambalo lilikubaliwa.

Alifika Chiromo kushuhudia operesheni hiyo chini ya usimamaizi wa maafisa wa polisi kutoka Gereza la Lang’ata ambako amekuwa akizuiliwa kwa muda sasa.

Miongoni mwa wanapatholojia watatu walioendesha upasuaji huo ni Johansen Oduor ambaye anawakilisha serikali, huku wengine wakiwakilisha jamaa za Cohen na Bi Wairimu.