Habari Mseto

Nitaangamiza ufisadi Kiambu, aapa Nyoro

December 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

UFISADI ni sharti liangamizwe kabisa katika kaunti ya Kiambu ili maendeleo yapatikane.

Haya ni kulingana na kaimu Gavana Dkt James Nyoro, aliposema kaunti hiyo itapata mwongozo mpya katika uongozi wake.

Baadhi ya maswala na miradi muhimu anayopania kutilia mkazo wakati wa uongozi wake ni afya, maji miundo msingi ya barabara na elimu hasa ya chekechea (ECD).

“Tutatilia mkazo ya kurekebisha hospitali kama ya Thogoto, na Lari huku lengo likiwa ni kuongeza vitanda zaidi, na pia tukiongeza vifaa muhimu katika hospitali kubwa za kaunti ya Kiambu,” alisema Dkt Nyoro.

Aliyasema hayo mnamo Alhamisi wakati wa kuadhimisha Jamhuri Dei, katika Uwanja wa michezo wa Ndumberi, Kiambu.

Alisema kaunti ya Kiambu inaunga mkono maswala ya maridhiano ya BBI itaendelea kuwahamasisha wananchi ili waweze kuielewa inavyostahili.

“Sisi kama kaunti ya Kiambu tunaiunga mkono BBI kwa lengo la kuunganisha nchi kuwa kitu kimoja. Ni vyema kufuata wito wa raisi ili kuweka wakenya pamoja hata siku za hapo baadaye,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema wafugaji wa Ng’ombe wa maziwa wataendelea kunufaika huku akipania kufungua vituo 20 vya kupeleka maziwa katika kaunti hiyo.

Alisema soko zingine nne zitajengwa katika maeneo tofauti kupitia ufadhili wa mradi wa Benki ya dunia.

“Soko hizo ziko Kikuyu, Juja, Ruiru, Kinjara. Kuna lingine litajengwa Githurai lenye uwezo wa kuhifadhi wafanyi biashara wapatao 2,000.

Spika wa bunge la kaunti ya Kiambu Askofu Stephen Ndichu alisema mtu yeyote atakayeeneza chuki kwa kutoa matusi kwa viongozi atalazimishwa kuhama kutoka kaunti ya Kiambu.

“Mimi natoa ilani leo kuwa mtu yeyote yule atakayemtukana rais Uhuru Kenyata, Ruto, Raila, ama kiongozi yeyote hapa Kiambu tutalazimika kwa kauli moja kumfurusha asituletee upuzi hapa,” alisema Bw Ndichu.

Alisema serikali isiwabembeleze wafisadi bali ipambane nao bila huruma.

Mwakilishi wa wazee wa Mau Mau Bw Gitu Wa Kahengeri, alitaka watu waliopigania uhuru wa nchi hii wapewe heshima zao kwa sababu waliweza kumng’oa mbeberu kwa kumwaga damu.

“Tungetaka historia ya wazee wa Mau Mau iangaziwe kupitia maandishi huku akihimiza kaunti ya Kiambu kuchukua jukumu la kuandika historia hiyo na kuiweka kwenye makavazi,” alisema Bw Kahengeri.

Aliwahimiza wakenya popote walipo wamuunge mkono rais Uhuru Kenyatta kwa juhudi zake za kuangazia maswala ya BBI.

“Tunataka kuona Kenya iliyo ya umoja na ushikamano miongoni mwa makabila yote ya nchi. Kwa hivyo mtu yeyote anayependa nchi hii anastahili kuunga mkono BBI,” alisema Bw Kahengeri.

Gavana mshikilizi wa Kiambu Dkt james Nyoro kulia, wakiwa na Spika wa kaunti ya Kiambu, Askofu Stephen Ndichu wakati wa kuadhimisha Jamhuri Dei katika uwanja wa Ndumberi Kiambu.