NLC kuwafidia wakazi wa Gatundu Kaskazini kwa ardhi ya ekari 300
Na LAWRENCE ONGARO
WAKAZI wa Gatundu Kaskazini wana jambo la kutabasamu baada ya serikali kuanza kuwalipa fidia ya ardhi yao.
Serikali inapanga kujenga bwawa la maji la thamani ya Sh24 bilioni kwenye ardhi la ekari 300 la Kariminu.
Hivi majuzi mwenyekiti wa Tume ya Ardhi nchini (NLC), Profesa Mohammed Swazuri, alizuru eneo hilo na kuwapa mpangilio jinsi fedha za fidia zitaendelea kulipwa wakazi wa eneo hilo.
Wakazi wa Gatundu Kaskazini watakaofaidika na mpango huo ni kutoka kijiji cha Kanyoni, Buchana, na Kiriko, huku wakitarajia kupokea kitita cha Sh 1.286 bilioni.
Mkutano wa hadhara ulifanyika eneo la Kiriko ulijumuisha wakazi zaidi ya 2,000 ambao watalazimika kuhama ardhi yao na kutafuta kwingine pa kuishi.
Wakati wa mkutano huo kila mkazi alipokea barua iliyoandikwa masharti fulani ili uweze kuwa kwenye orodha ya watakaolipwa fidia.
Barua hiyo ilieleza kuwa mhusika amekubali kupeana ardhi yake kwa serikali ili mradi wa bwawa la maji lijengwe hapo.
Maswala mengine kwenye barua hiyo ilikuwa ni jina mhusima na baadhi ya mali muhimu aliyokuwa nazo kabla ya kuhama.
Barua hiyo pia ilieleza kiwango cha fedha mhusika alitarajia kupokea kabla ya kuhamia kwingineko.
Mradi huo wa maji unatarajia kujengwa kwenye eneo la ekari 300 la ardhi huku likitarajiwa lianze kazi haraka iwezekanavyo.
Wakazi hao walijulishwa ya kwamba baada ya wao kutia saini stakabadhi hizo fedha zao zitawasilishwa katika akaunti zao za benki mara moja.
“Baada ya wiki moja hivi kila mmoja aliyetia saini barua yake atapokea kitita chake kwenye benki. Kwa hivyo hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi wowote,” alisema Prof Swazuri.
Alisema awamu ya pili ya mradi huo unastahili kuzinduliwa mara moja, lakini itachukua muda kidogo kwa sababu wengi wa wakazi hao hawajawasilisha mambo yote muhimu inayohitajika.
Hata hivyo walihakikishiwa kuwa watapewa muda wa kujipanga kuhamia kwingineko kabla ya serikali kuingia katika ardhi yao.
Mwenyekiti wa kamati ya kuwasilisha majina hayo Bw Paul Maina alikiri kuwa kila mkazi alipata ujumbe kuhusu kuhamishwa mahali hapo na kwa hivyo hakuna yeyote aliye na malilio yoyote.
“Kila mmoja amewasilisha ardhi yake kwa serikali bila kushurutishwa na kwa hivyo walikubali mradi huo ufanyike hapo,” alisema Bw Maina.
Hata hivyo alisema ni muhimu kuwahamasisha wananchi jinsi ya kutumia fedha hizo ili ziweze kuwanufaisha na familia zao. ni vyema kufanya kazi kwa mpangilio unaostahili,” alisema Bw Maina.
Naibu kamishna wa Gatundu Kaskazini, Bw Brexton Mayambi, alisema hali ya usalama umeimarishwa kikamilifu ili kuepuka ulaghai ambao unaweza kutokea.
“Ninawahimiza wale watapata fedha zao wazipeleke katika benki ili watumia kadi ya ATM kila mara wanapokwenda kutoa pesa. Mtu yeyote hafai kuweka fedha zake nyumbani kwa sababu ni hatari kwa usalama wake,” alisema Bw Mayambi.