Habari Mseto

Nondies kuhamia uwanja mpya

June 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

WANARAGA wa klabu ya Nondies sasa watakuwa wakisakata mechi zao za nyumbani katika uwanja wa Jockey Club of Kenya badala ya uwanja wa maonyesho ya Jamhuri.

“Kwa niaba ya klabu, tuna fahari ya kutangaza kuwa tumetia saini mkataba wa miaka 10 itakayorefushwa baadaye na Jockey Club of Kenya na sasa tutahamia katika eneo la Racecourse, Nairobi,” ikasema sehemu ya taarifa ya Nondies.

Kwa mujibu wa meneja wa Nondies, Kevin Were, kikosi chake kimepanuka zaidi na kwa sasa uwanja wa Jamhuri hauna uwezo wa kuwawezesha kufaulisha mingi ya mipango yao.

“Ingawa uwanja huo umetupa jukwaa zuri la kuandalia mechi nyingi, uga mpya ambao tumepata ni mwafaka zaidi kwa kuwa ni mkubwa na utatupa fursa bora zaidi za kujipatia riziki kwa minajili ya kuwadumisha wachezaji na maafisa kimshahara na kuendesha kikosi,” akasema.

Were amefichua kwamba kingine kilichowachochea kubanduka uwanjani Jamhuri ni mpango wa ASK kutaka kupanua shughuli za biashara katika uga huo.

“Uwanja wa Jockey Club of Kenya umefikia viwango vya kimataifa. Kwa sasa upo katika hatua za mwisho za ukarabati na utatoa jukwaa zuri mno kwa wachezaji,” akasema Were.

Hii ni mara ya nne kwa kikosi cha Nondies ambacho ndicho cha zamani zaidi katika raga ya Kenya kuhama. Nondies walicheza kwa takriban miaka 13 katika uwanja wa Parklands Sports Club Nairobi kabla ya kuhamia St Mary’s School kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Mnamo 2003, kikosi hicho kilihamia katika uwanja wa maonyesho wa Jamhuri Park ambao wamekuwa wakitumia kwa pamoja na Homeboyz RFC.

Mnamo Mei 2020, Nondies walisuka upya benchi ya kiufundi ya kikosi chao kwa kumwajiri nyota wa zamani wa kimataifa na kocha wa timu ya taifa ya chipukizi wa U-20, Michael Aung kusaidiana na wakufunzi Kenny Andola na Hillary Itela.

Kocha mkuu Willis Ojal ameelezea matumaini yake kwamba kikosi chake cha Nondies kitafuzu kwa mchujo wa Ligi Kuu ya Kenya Cup msimu ujao. Nondies walikamilisha kampeni za msimu huu katika nafasi ya nane jedwalini.