• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 9:35 AM
Nyadhifa za uongozi Jubilee Party kung’ang’aniwa mwaka 2020

Nyadhifa za uongozi Jubilee Party kung’ang’aniwa mwaka 2020

Na MWANGI MUIRURI

MRENGO wa Naibu Rais Dkt William Ruto unadadisiwa kuwa unajipanga kuchukua udhibiti wa chama cha Jubilee mapema mwaka 2020 mnamo wakati ambapo maafisa wanaoshikiklia nyadhifa za uongozi katika chama hicho tawala wanatarajiwa kuachia nafasi hizo Mei 2020.

Mrengo huo wa Dkt Ruto unanuia kufanyia mabadiliko mpangilio wa chama cha Jubilee katika nyanja za maamuzi ili kumwondoa Rais na washirika wake kutoka nafasi ya kushawishi uamuzi wa mrithi ndani ya chama hicho.

“Rais anang’atuka mamlakani mwaka 2022 na sheria tulizo nazo kwa sasa hazimpi nafasi ya kuwania wadhifa mwingine wowote. Amekuwa akikiri hadharani kuwa hana haja ya kusalia mamlakani kama anavyoshinikizwa na baadhi ya wanasiasa; kumaanisha anafaa kuenda nyumbani akapumzike nasi tulio na ajenda za kisiasa za baada ya mwaka 2022 tushike usukani chini ya unahodha wa Dkt Ruto,” asema aliyekuwa mwenyekiti wa wawaniaji wa Jubilee Mlima Kenya, Samuel Maina.

Maina anadai huu ni msimu wa siasa, Wakenya hawachoki na siasa na “wanazipenda huku nasi tukiwa ni wanasiasa ambao huwezi ukatuzima kuendeleza mikakati yetu ya kujipanga.”

Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu aliambia Taifa Leo kwamba wana mipango ya kujiimarisha kama chama.

 “Tunaweka wazi ajenda yetu ya kumuunga mkono Ruto na ndiyo sababu tunataka Rais awe tu wa kutushauri kama aliye na tajiriba ya uongozi nasi tuchukue usukani wa mieleka nyanjani kuhusu urithi ifikapo 2022,” akasema Waititu.

Hana mamlaka

Tayari, mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, mwenzake wa Bahati Kimani Ngunjiri na Kimani Ichung’wa wa Kikuyu wamesikika wakisema kuwa Rais hana mamlaka ya kuzima Wakenya kujadiliana kuhusu kesho yao ya kisiasa.

Pia, Dkt Ruto mwenyewe akiwa katika eneo la Eldama Ravine alisema hakuna ubaya wowote kwa “sisi kujipanga kuhusu uchaguzi mkuu wa 2022.”

“Hata Wakristo kwa sasa wanajiandaa kwa safari ya mbinguni hata ikiwa hatujui siku wala saa ya kutimia kwa safari hiyo,” alisema Ruto.

Aidha, alishasema chama cha Jubilee kitaandaa mkutano wa pamoja wa kujipanga.

Bw Albert Nyaundi akiwa ni mwanakamati katika bodi ya ushauri wa chama alithibitishia Taifa Leo kuwa kipengele cha awamu ya uongozi ndani ya chama hicho kinatoa mwanya wa uchaguzi wa maafisa wapya mwaka 2020.

Bodi hiyo ya ushauri huwa na maafisa wanaowakilisha vyama 12 vilivyouingana 2017 kuunda chama cha Jubilee.

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi aliambia Taifa Leo kuwa “tunaisubiri siku ya uchaguzi wa chama kwa hamu kuu ndio tujiweke kama chama kilicho na serikali kwa sasa na kinacholenga kuendeleza malengo ya chama ya kusalia mamlakani.”

Alisema kuwa kwa sasa kuna orodha ya watakaowekwa katika nyadhifa za chama wakijumuishwa katika makundi manane yanayozingatia Mikoa ya kabla ya Katiba Mpya kuunda majimbo 47.

“Tunalenga kuwa na majenerali wa chama katika ngome zetu za Mlima Kenya na Rift Valley kisha tudhibiti Nairobi, Pwani na Kaskazini Mashariki kabla ya kujiweka pema katika eneo la Magharibi. Lengo letu ni kuwindana na kinara wa ODM Raila Odinga ambaye ndiye mpinzani wetu mkuu huku tukiondoa sauti za uasi ndani ya chama chetu cha jubilee,” akasema Sudi.

  • Tags

You can share this post!

WASIA: Ukiitumia vyema likizo unaweza kubadili kabisa...

SEKTA YA ELIMU: Sababu zinazochangia kushuka kwa utendakazi...

adminleo