Nyandarua yasifiwa kutilia maanani kanuni za Covid-19
Na SAMMY WAWERU
Nyandarua ni kati ya kaunti 9 ambazo hazijaandikisha maambukizi ya Covid – 19, tangu kisa cha kwanza cha ugonjwa huu kiripotiwe nchini mnamo Machi 13, 2020.
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe Jumatatu katika ziara yake Nyandarua kukagua maandalizi ya kaunti hiyo dhidi ya corona, amewataka wakazi kuendelea kujizuia kuambukizwa.
“Nyandarua ni miongoni mwa kaunti 9 kwa jumla ya 47, ambazo hazijaandikisha Covid – 19,” Bw Kagwe akasema.
Alidokeza kwamba sampuli 600 kutoka Nyandarua zimefanyiwa ukaguzi na vipimo, na hakuna aliyepatikana na virusi vya corona.
“Hata hivyo, hiyo haimaanishi watu wa Nyandarua hawawezi kuambukizwa. Ninawahimiza muendelee kutilia maanani sheria na mikakati iliyowekwa kuzuia maambukizi. Hii ndiyo kaunti ambayo nimetembea na kila mtu amevalia barakoa,” Waziri Kagwe akaeleza.
Akipongeza wakazi, alisema uzingatiaji wa mikakati kuzuia msambao wa Covid – 19, utaondolea familia hatari ya kugonjeka na gharama ya matibabu, ikiwa ni pamoja na kuipa nafuu serikali za kaunti na serikali kuu, fedha zinazotumika kwa shughuli hiyo zielekezwe katika miradi ya maendeleo.
Aidha, Bw Kagwe alipongeza wahudumu wa afya Nyandarua, kwa kile alitaja kama kujitolea mhanga kuhudumia wananchi wa humo kutokana na taswira iliyomkaribisha katika vituo mbalimbali vya afya.
Wakati huohuo, Jumatatu, katika kipindi cha saa 24 zilizopita Kenya imethibitisha maambukizi mapya 133 kutoka kwa sampuli 3,365, idadi jumla ya wagonjwa wa Covid – 19 ikifikia 3,727.
Kufikia sasa, jumla ya sampuli zilizofanyiwa ukaguzi na vipimo ni 118,701.
Akitoa takwimu hizo, Waziri Kagwe pia alisema wagonjwa 33 wameruhusiwa kuenda nyumbani baada ya kuthibitishwa kupona, idadi jumla ya waliopona ikifika 1,286.
Mgonjwa mmoja ametangazwa kuangamia kutokana na Covid – 19, kisa hicho kikifisha 101 walioafariki kutokana na ugonjwa huu hatari.