• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Nyani wateka ploti, waiba, kucharaza na kutimua wapangaji

Nyani wateka ploti, waiba, kucharaza na kutimua wapangaji

PURITY KINUTHIA NA RICHARD MAOSI

WAKAZI wa mitaa ya Nakuru wameshindwa kuvumilia mahangaiko ya kuvamiwa, kuibiwa na kucharazwa na nyani wakorofi.

Mara hii nyani hao wanawalenga akinamama, watoto na wamiliki wa nyumba za kupangisha zinazopatikana karibu na Mbuga ya Kitaifa ya Wanyama ya Ziwa Nakuru.

Mitaa ya Bondeni, Freearea, Murogi, Manyani, Flamingo na Lakeview imesajili visa hivi kwa wingi.

Kwa zaidi ya miaka 10, nyani wamegeuka kero kwa wamiliki wa vyumba vya kupangisha, kwa kuharibu mali zao au kuwaibia jambo linalowatia wapangaji hofu.

Elizabeth Kahura Thiongo kutoka mtaani Freearea anasema aliamua kuwekeza kwenye mradi wa nyumba za kupangisha mara tu baada ya kustaafu.

Hata hivyo, nusura akate tamaa alipogundua nyani wakorofi, ambao hapa wanajulikana kama ‘cops’ walikuwa wakipiga doria katika ploti yake kila siku, utadhani ndio wamiliki.

Katika mahojiano na Taifa Leo, asema alinunua kipande hiki cha ardhi mnamo 1982.

Awali alitumia shamba lake kukuza viazi na mahindi ila mambo yalibadilika ilipofika 1996, nyani kutoka Mbuga ya Ziwa Nakuru walipoanza kuendesha shughuli katika ploti yake.

“Nilipojenga nyumba za kupangisha sikujua nitaanza kupitia changamoto hizi ila hali ilizidi kuwa mbaya idadi ya nyani zilipoendelea kuongezeka,”asema.

Anasema kwa kawaida nyani huvunjavunja paa na wakati mwingine kuvamia mashamba wakisaka chakula.

Kwa ufundi mkubwa, wao hutumia kucha zao kutenganisha mabati na misumari, kisha wakaingia chumbani kunyaka chochote wanachopata.

Cha kuvunja moyo ni kwamba maafisa wanaosimamia wanyamapori hawajaweka mikakati yoyote kudhibiti viumbe hawa jambo ambalo lilifanya Bi Kahura kutumia Sh30,000 kuzungushia ua wa umeme.

“Hatua hiyo ilinigharimu Sh2,500 kila mwezi kugharamia umeme kwenye Shirika la Kusambaza Umeme Nchini KPLC.”

Ni kwa sababu hiyo ambapo wapangaji wengi wameamua kugura makwao na kuelekea kwingine ili kunusurika mahangaiko yasiyokoma.

Bi Jane Ngina ambaye ni landilodi anasema nyumba zake zimebaki tupu wapangaji waliposhindwa kukesha wakilinda nyumba zao hasa nyakati za mchana.

“Aidha, wapangaji hawawezi kuacha milango au madirisha yakiwa wazi kwani nyani hunyatia polepole na kusaka chakula katika kila sehemu ya nyumba na kuacha vyombo vikiwa vimetapakaa,” asema.

Kwa Elizabeth Nyandia, siku moja nyani walitafuna kuku wake hadharani.

Anasema alikuwa amechukua mkopo wa Sh200,000 kuanzisha mradi huo ila siku moja alishtuka, nyani walipovamia kibanda cha kuku wake kisha wakatorokea paani wakiwa na kuku.

Sospeter Gichimu anasema maeneo husika yamekuwa yakibakia nyuma kimaendeleo kwa sababu ya visa kama hivi.

Kwa upande mwingine, Elizabeth Muthoni anasema mnamo 2022 alipigwa na nyani kwenye mkono wake na ikabidi afanyiwe upasuaji ili kutibu mkono wake uliokuwa ukivimba.

Alikaa kwa zaidi ya mwaka mmoja bila kufanya kazi na hivyo basi kuwategemea wahisani jamaa na marafiki kufanya kazi za ndani.

Bw Cheruiyot Chepkwony afisa msimamizi wa Wanyama pori Kaunti ya Nakuru anasema kulingana na sheria za kudhibiti wanyamapori, nyani hawachukuliwi kama mojawapo.

“Sheria hii iliyopitishwa na wabunge haitoi nafasi kwa walalamishi kufidiwa hii ikimaanisha kwamba siku za baadae sheria kama hii itaangaziwa.

Anasema kilomita 78 ya waya wa umeme unaozunguka Ziwa Nakuru imekarabatiwa na kubadilishwa na waya wa kilomita 86 kupunguza visa vya makabiliano kati ya wanyama pori na binadamu.

  • Tags

You can share this post!

Mudavadi anavyocheza karata yake ya kisiasa chini ya maji

Vitunguu, dhahabu ambayo bei yake sasa haikamatiki

T L