Nyanya wa miaka 81 abakwa, amwagiwa asidi kisha kuuawa
Na WAANDISHI WETU
NYANYA mwenye umri wa miaka 81 kutoka kijiji cha Kihumbuini, Gatanga katika Kaunti ya Murang’a alinajisiwa kabla ya kuuawa, kisha mwili wake ukamwagiwa asidi katika kile wenyeji wametaja wanashuku ni kuhusu mzozo wa ardhi.
Mwili wa Lydia Wanjiku Chege ulipatikana uchi wa mnyama siku ya Jumatatu mita 500 kutoka nyumba yake ukiwa umelowa damu.
Mzee Stephen Ng’ang’a, ambaye alikuwa kati ya wanakijiji waliomwona nyanya huyo akiwa katika hali hiyo ya kutisha, alisema kwamba walifikiria alikuwa amefariki ila wakagundua bado alikuwa hai ndipo wakaita polisi waliompeleka hadi hospitali ya Thika Level Five.
Kabla ya kufariki kutokana na majeraha, mwanamke huyo aliweza kusimulia jinsi alivyodhulumiwa na waliohusika kumuacha mahututi wakidhani amekufa.
“Alikuwa na uchungu mwingi japo alijilazimisha kuzungumza na kusema kwamba amewasamehe waliomvamia. Tulimpa moyo kwamba atapona lakini Jumatano jioni tulipata taarifa kwamba ameaga dunia,” akasema Bw Ng’ang’a.
OCPD wa Gatanga, Beatrice Kiraguri aliwaomba wenyeji kutochukua sheria mikononi mwao na kulipiza kisasi mauaji hayo. Alifichua kwamba wameanzisha uchunguzi kuhusu kisa hicho ingawa kufikia jana jioni hawakuwa wamemkamata mshukiwa yeyote.
“Marehemu alikuwa ameandikisha taarifa nasi na kutoa maelezo kuhusu sura na maumbile ya waliomdhulumu. Tumeanzisha uchunguzi na tunawaomba wenyeji wasichukue sheria mikononi mwao,” akasema Bi Kiraguri.
Katika kaunti jirani ya Kirinyaga, mwanaume amelazwa katika hospitali ya Kimbimbi baada ya mkewe kummwagia maji moto kutokana na SMS ya mapenzi aliyotumiwa na mwanamke mwingine.
Kulingana na majirani, mwanaume huyo alipiga nduru baada ya kumwagiwa maji hayo na kuvutia majirani waliofika na kumpeleka hospitalini huku mkewe akitoroka. Polisi bado wanamsaka mwanamke huyo.
Kwingineko, wanakijiji waliojawa na ghadhabu walimpiga hadi kufa mwanaume aliyemuua babake baada ya kuzozania Sh100 katika kijiji cha Kalyet, Elburgon, Kaunti ya Nakuru mnamo Jumatatu usiku.
Kulingana na chifu wa eneo hilo Harrun Koima, mshukiwa Erick Kibiwot, 30, alivamiwa na wanakijiji alipokuwa akirejea nyumbani kutoka mafichoni.
Mkuu wa polisi wa Molo, Kioko Muinde alikashifu mauaji hayo na kuwaomba vijana kuwaheshimu wazazi wao.
Katika Kaunti ya Isiolo, mwanamume aliyetambuliwa kama Nginai Lemantaan, 51, kutoka kijiji cha Kipsing aliuawa baada ya kukataa bintiye awachungie washukiwa mbuzi, akisisitiza kwamba alifaa kuwa shuleni kuendeleza masomo yake.
Uamuzi huo unadaiwa uliwakasirisha washukiwa hao ndipo wakamdunga kisu na akafariki alipokuwa akifikishwa katika hospitali ya Kaunti ya Isiolo.
Naibu chifu wa Kipsing, Rambei Lekipaika alithibitisha kisa hicho.
Taarifa za Ndung’u Gachane, George Munene, John Njoroge na Vivian Jebet