Habari Mseto

Nyoro azimwa na korti kutimua mawaziri Kiambu

September 26th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

NAIBU Gavana katika Kaunti ya Kiambu, Bw James Karanja Nyoro, ameagizwa na mahakama kuu akome kuwafuta kazi mawaziri walioteuliwa na Gavana Ferdinand Waititu, aliyeshtakiwa kwa madai ya ulaghai na kashfa ya Sh588 milioni.

Jaji Onesmus Makau alimwamuru Bw Nyoro akome mara moja kufanya uteuzi wa maafisa wakuu wa kaunti hiyo kwa vile hana mamlaka ya kutekeleza majukumu hayo, hadi wakati kesi inayompinga kuchukua hatua hizo itakapoamuliwa.

Agizo hilo limemzuia pia kuwatimua kazini vibarua zaidi ya 1,000.

Jaji huyo alikataa ombi la Bw Nyoro kutaka maagizo yoyote yasitolewe kwa vile kuna kesi sawa na hiyo mbele ya mahakama ya rufaa na mbele ya Jaji Weldon Korir itakayosikizwa Oktoba 4, katika mahakama kuu Nairobi.

“Bw Nyoro alikaidi vifungu nambari 32(4)(5) na 46 vya sheria ya kaunti kwa kuwatimua kazini vibarua 1,000 na kumhamisha Waziri wa Fedha Bw Francis Kigo Njenga,” anasema Bi Marion Njeri Njoroge mpiga kura aliyemshtaki Bw Nyoro.

Pia anadai Nyoro alimteua Bw David Njuguna Burugu kuwa mkuu wa wafanyakazi wa kaunti.

“Nyoro hana mamlaka kisheria kumfuta kazi au kumwachisha kazi afisa yeyote wa kaunti hiyo kwa vile anakaidi kifungu nambari 32 cha sheria za kaunti zinazomtwika gavana mamlaka ya kuwateua mawaziri na wakuu wa idara za kaunti,” alisema Jaji Makau.

Jaji huyo alimwagiza Bw Nyoro akome kuwahamisha wafanyakazi wakuu katika kaunti hiyo kutoka idara moja hadi nyingine.

Mahakama ilimwamuru asiwateue mawaziri wapya, kuwaachisha kazi wafanyakazi ama kuvuruga baraza la mawaziri walioteuliwa na Bw Waititu aliyeshtakiwa pamoja na mkewe Susan Wangari kwa upokeaji kwa njia ya ulaghai zaidi ya Sh50milioni kutoka kwa kampuni moja iliyopewa kandarasi ya kutengeneza barabara , wakijua zimetoka kwa serikali ya kaunti ya Kiambu.

Mahakama ilimwamuru Bw Nyoro asiwaingilie mawaziri, maafisa wa utekelezaji ama kuwavuruga maafisa wakuu waliokuwa wameteuliwa na Bw Waititu.

Wakili Nelson Masaviru aliyewasilisha kesi hiyo mbele ya Jaji Makau kwa niaba ya mkazi na mpiga kura wa Kiambu, Bi Njoroge alisema tangu naibu huyo wa gavana atwae hatamu za afisi hiyo ya Gavana, zaidi ya vibarua 1,000 wametimuliwa kazini na “ameanza kufanyia baraza la mawaziri mabadiliko.”

Bi Njoroge amemshtaki Bw Nyoro na Kaunti ya Kiambu akisema naibu huyo wa gavana hana mamlaka yoyote kisheria kuwaachisha kazi mawaziri waliokuwa wameteuliwa na Gavana Waititu.

Anasema katika kesi hiyo kwa Bw Nyoro aliteuliwa chini ya Kifungu nambari 179 (5) cha Katiba na Gavana Waititu.

“Bw Nyoro amekaidi sheria na katika siku za hivi punde amefanyia mabadiliko baraza la mawaziri kinyume cha sheria ikitiliwa maanani jukumu hilo ni la gavana,” alisema Bw Masaviru.

Jaji Makau aliratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuamuru isikizwe wiki ijayo ndipo kaunti ya Kiambu ikabidhiwe nakala hiyo ya kesi.