Nyumba 40 zilizojengwa kwa ardhi ya KPA kubomolewa
MOHAMED AHMED na KALUME KAZUNGU
TAKRIBAN nyumba 40 ambazo zimejengwa katika ardhi za bandari ya Mombasa ambazo zimenyakuliwa pamoja na zilizopo karibu na minara ya kuelekeza meli, zitabomolewa.
Zoezi la ubomozi wa nyumba hizo litafanyika katika muda wa wiki mbili zijazo na linatazamiwa kuathiri familia zaidi ya 40.
Tume ya ardhi za Kitaifa (NLC) imesema kuwa vipande vya ardhi 37 vya vinavyomilikiwa na halmashauri ya bandari vimenyakuliwa na watu kujenga ndani yake kinyume cha sheria.
Katika mahojiano na Taifa Leo, mwenyekiti wa NLC Muhammad Swazuri, alisema kuwa tume hiyo pamoja na serikali ya kaunti ya Mombasa zitabomowa nyumba 25 ambazo ziko kwenye ardhi hizo bandari na nyingine 15 ambazo zimejengwa karibu na minara hiyo ya baharini.
“Tuliwahi kutoa notisi mwaka jana na kuwaelekeza watu ambao wapo kwenye ardhi hizo waondoke. Muda huo umekishwa na kwa sasa kilichosalia ni watu hao kuondolewa,” akasema Prof Swazuri.
Alisema kuwa baadhi ya nyumba hizo ni pamoja na zile ambazo zipo kwenye ufuo wa bahari ya Shelly eneo la Likoni.
Nyumba hizo pia zimejengwa karibu na minara hiyo zipo kwenye eneo hilo la Likoni kaunti ya Mombasa katika mkondo wa bahari wa kivuko cha Likoni.
Nyumba za kifahari katika kaunti ya Kilifi pia ni miongoni mwa zile ambazo zinaziba kuonekana vyema kwa minara hiyo na kuhatarisha usalama wa meli hizo zinazoingia kwenye bandari ya Mombasa.
“Mabati ya nyumba ambazo zipo kwenye minara hiyo ndiyo yanafanya mwangaza kwenye taa za minara kutong’aa inavyofaa. Imekuwa shida kwa manahodha kuendesha meli zao wakati wanapoingia kwenye maji yetu,” akasema Prof Swazuri.
Mpango wa ubomoaji huo wa nyumba hizo unafanyika siku chache baada ya serikali ya kaunti ya Mombasa kuanza kubomoa zisizo salama kwa makazi.
Kwengineko katika kaunti ya Lamu, polisi wamelaumiwa kwa kumpiga mwanamke na kumuumiza.
Bi Mariam Wanjiru, 43, mkazi wa kijiji cha Manda, anadai kupigwa na kuumizwa na polisi wakati akitoka dukani kununua bidhaa.
Anasema alikuwa ameandamana na watoto wake watatu, alipocharazwa na polisi hao wanaodaiwa kumwangusha chini, na kumsababishia majeraha ya shingo na mashavu.
Bi Wanjiru anayetibiwa katika hospitali kuu ya King Fahad mjini Lamu, anasema alinyimwa a fomu ya matibabu (P3) kutoka kituo cha polisi cha Lamu.
“Nilikuwa nimetoka dukani kununua bidhaa.
Ilikuwa saa mbili usiku. Nilikuwa nimeandamana na watoto wangu. Ghafla polisi wanne walitujia na kuanza kunipiga na kuniangusha chini. Waliniumiza shingo yangu na mashavu na tayari nimetibiwa hapa hospitalini King Fahad. Nimejaribu kutafuta P3 kituoni lakinio kila ninapofika ninazungushwa. Ninahitaji msaada ili nipate haki,” akasema Bi Wanjiru.
Dadake Mwathiriwa, Bi Miriam Njeri, aliambia Taifa Leo kwamba visa vya polisi kuwapiga na kuwaumiza ovyo wakazi eneo la Manda vimekithiri mno.
Bi Njeri aliwaomba wakuu wa usalama Lamu kuwachunguza wadogo wao kwa kuendeleza ukiukaji wa haki za binadamu kila wanapokuwa kazini.
“Polisi wanafaa kutulinda badala ya kutuumiza sisi raia. Dadangu tayari ni mgonjwa wa moyo na tangu tukio hilo, hajarejelea hali yake ya kawaida,” akasema Bi Njeri.
Hiki ni kisa cha pili cha polisi kuwapiga na kuwajeruhi raia katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, kaunti ya Lamu.
Wiki jana, familia moja ilijitokeza kudai haki kwa kijana wao aliyepigwa na kuumizwa vibaya na poliosi eneo la Ndau, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki.
Bw Yusuf Abuu,19, alipigwa na kuumizwa matumbo yake, hatua ambayo ilipelekea yeye kufanyiwa upasuaji wa nyongo yake kwenye hospitali hiyo ya King Fahad.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi wa Kaunmti ya Lamu ili kuzungumzia suala hilo ziligonga mwamba kwani hakupokea simu.