Habari Mseto

Nzige: Mwinjilisti asema Mungu amekasirishwa na Kenya

February 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

MENGI yamesemwa kuhusu mabilioni ya nzige ambao wamekuwa yakihangaisha Wakenya na wakazi wake kwa miezi miwili sasa tangu wawasili Desemba 28, 2019, wakitokea Somalia.

Hata hivyo, serikali inapoendelea kukabiliana na wadudu hao waharibifu wakati huu wakulima wanaanza kuandaa mashamba kwa msimu wa upanzi, swali ni je, kanisa linasimama wapi katika mjadala huu wote?

‘Taifa Leo’ imezungumza na mwinjilisti Alphonce Wandera ambaye ni Askofu.

“Mungu amekasirishwa na Kenya,” anasema Wandera na kuongeza kuwa tangu enzi za Biblia, nzige (na hata magonjwa) walikuwa wakiachiliwa na Mungu kuadhibu binadamu walipokuwa wamemkasirisha kwa kuzama katika dhambi.

Wandera anasema kuwa watumishi wa Mungu nchini Kenya ndio wakulaumiwa zaidi kwa nzige kuingia humu nchini kwa sababu wamepoteza mwelekeo.

“Watumishi wa Mungu wameenda kinyume na neno la mungu. Hawafundishi ukweli,” anasema Askofu huyo wa kanisa la Worship Land Miracle Church lililo na matawi matano katika kaunti ya Nairobi.

Suluhisho, anasema, ni Wakenya kutubu, kuomba msamaha na kurejea kwa Mungu ndipo Kenya ipate kuponywa.

Tangu Desema 2019, nzige wamevamia karibu kaunti 25 zikiwemo Mandera, Wajir, Garissa, Isiolo, Samburu, Meru, Laikipia, Marsabit, Kirinyaga, Turkana, Tharaka-Nithi, Kitui, Machakos, Embu, Kisumu, Baringo, Nyeri, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, West Pokot na Migori.

Wameharibu mimea mingi na tani ya vyakula shambani na kuweka Kenya katika hatari ya kushuhudia baa la njaa.

Mwinjilisti Alphonce Wandera ambaye ni Askofu. Picha/ Geoffrey Anene

Mwezi Januari, Waziri wa Kilimo Peter Munya alisema itachukua karibu miezi sita kudhibiti nzige hao wa jangwani, ambao pia wanahangaisha mataifa ya Ethiopia, Somalia, Djibouti, Eritrea, Uganda, Sudan Kusini na Tanzania.

Ni mara ya kwanza kwa zaidi ya miaka 70 Kenya imeshambuliwa vibaya na wadudu hao, ambao husafiri kilomita 150 kwa siku. Kundi moja la nzige linasemekana linaweza kutafuna chakula ambacho ndovu 10 ama ngamia 25 ama watu 2,500 wanaweza kutia tumboni kwa siku moja.

Jinsi Kenya imekuwa ikikabiliana na nzige

Mwezi Januari, serikali ya kaunti ya Wajir iliamrisha polisi kutumia vitoa machozi kukabiliana na wadudu hao. Pia, ilishauri wakazi wa eneo hilo kupiga kelele kama mojawapo ya njia za kumaliza wadudu hao waharibifu. Katika kaunti zilizoathiriwa, Wakenya pia wamekuwa wakitumia mbinu zao kufurusha wadudu hao.

Waziri Munya pia alinukuliwa Januari akisema kuwa wizara hiyo inatumia njia za kisayansi kukabiliana na nzige ikiwemo kuwanyunyuzia kemikali za kuua wadudu. Ndege zimekuwa zikitumika katika shughuli ya kunyunyiza dawa hizo kutoka angani. Wizara yake imetenga Sh232.7 milioni kupiga jeki vita dhidi ya nzige.

Aidha, wataalamu wa lishe bora walinukuliwa majuzi wakitaka Wakenya wavune nzige hao, wawakaushe na kuwala.

Kwa maoni ya Askofu Wandera, hata hivyo, nzige wanaoshuhudiwa nchini Kenya hawafai kuliwa kwa sababu wamekuja kuharibu na wala si kama chakula.