‘Nzige watachangia utapiamlo katika jamii za wafugaji’
Na JACOB WALTER
WANAWAKE na watoto ndio wameathiriwa zaidi na athari za uvamizi wa nzige nchini, Shirika la Msalaba Mwekundu nchini (KRC) limesema.
Katibu Mkuu wa shirika hilo, Dkt Asha Mohammed alisema hayo kwenye ripoti ya kutathmini athari za uvamizi wa wadudu hao waharibifu nchini.
“Tayari tumewasilisha ripoti kuhusu uvamizi wa nzige kwa Wizara ya Kilimo na Shirika la Kilimo Ulimwenguni (FAO) na itachapishwa hivi karibuni,” Dkt Mohammed alisema.
Alikuwa akizungumza alipotembelea gavana wa Marsabit, Mohammed Ali mnamo Jumatatu.
Alisema kwamba wanawake na watoto ni miongoni mwa walioathiriwa na majanga katika jamii hasa kwa kukosa lishe bora.
Dkt Mohammed alisema kwamba, jamii za wafugaji katika maeneo kame zimeathiriwa na uvamizi wa nzige ambao waliharibu mimea.
Alitaja kaunti za Marsabit, Samburu, Turkana na Isiolo kama zilizoathiriwa pakubwa na nzige na wadudu hao wangali wanaendelea kusambaa na kuharibu mimema.
Alisema kwamba, ripoti hiyo na mapendekezo yaliyomo zitawezesha serikali na wadau wengine kubuni mikakati ya kukabili uvamizi wa nzige siku zijazo.
Aliongeza kuwa ripoti hiyo itasaidia serikali kuamua mfumo wa kufidia wakulima na wafugaji katika maeneo yaliyoathiriwa ili waweze kuanza upya maisha yao.
Dkt Mohammed alisema kwamba, shirika la Msalaba Mwekundu litaendelea kusaidia serikali kujiandaa kukabiliana na Nzige siku zijazo licha ya kuwa wameanza kupungua.
Gavana Mohamud Ali alisema wadudu hao walivamia nchi wakati inakabiliana na janga la Corona na juhudi zote zinaelekezwa kwa ugonjwa huo.
Gavana Ali alisema uharibifu uliosababishwa na wadudu hao unaweza kuchangia uhaba mkubwa wa chakula, ukosefu wa usalama na utapia mlo katika kaunti hiyo.
Aliomba serikali kuweka mikakati thabiti ya kulinda jamii za wafugaji ambao wanakabiliwa na tisho la njaa kutokana na uvamizi wa Nzige.
“Inasikitisha juhudi nyingi zilielekezwa kuzuia corona huku uvamizi wa nzige na shida nyingine zikisahaulika,” alisema Gavana Ali.
Uchunguzi kuhusu athari za uvamizi wa nzige ulianza Juni 15, 2020 na ulifanywa katika kaunti 16.Ripoti ya mwisho ilitarajiwa Julai 15, 2020.
Shirika la Msalaba Mwekundu lilipatiwa kazi ya kufanya uchunguzi huo na FAO kwa gharama ya Sh42 milioni.
Lengo la uchunguzi huo ni kusaidia serikali ya Kenya kutathmini kiwango cha uharibifu, idadi ya watu walioathiriwa na sehemu iliyoathiriwa na wadudu hao.