• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Obado akiri kupotosha wakazi kuhusu corona

Obado akiri kupotosha wakazi kuhusu corona

Na IAN BYRON

GAVANA wa Migori, Okoth Obado amewaomba msamaha wakazi wa kaunti hiyo kwa kuwataka wasizingatie masharti ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona miezi mitatu iliyopita.

Bw Obado mnamo Septemba aliwataka wakazi wa Migori wasivae barakoa na kutozingatia hitaji la kutokaribiana.

Akizungumza wakati wa kikao na kamati ya kupambana na virusi vya corona katika makazi yake, gavana huyo alijuta kwa matamshi yake, na akawarai wakazi wazingatie masharti yaliyowekwa na serikali.

“Lazima nikubali kwamba nilishauriwa vibaya kuhusu ugonjwa lakini sasa nishatambua makosa yangu. Sitaki mtu yeyote atumie matamshi yangu kudai kwamba virusi vya corona havipo. Nimegundua kweli kwamba ugonjwa huo upo. Wakati huo nilichanganyikiwa wala sikujua makali yake,” akasema Bw Obado.

Wakati huo Bw Obado na Kamishna wa Kaunti ya Migori, Boaz Cherutich walitofautiana hadharani katika hafla moja mjini Isebania, gavana huyo aliposema virusi vya corona havipo na ni ubunifu tu wa viongozi wachache.

Hata hivyo, Jumanne alibadili kauli na kuwataka wakazi wajilinde dhidi ya virusi vya corona kwa kufuata mwongozo uliowekwa na serikali.

“Kila mtu anafaa afahamu kwamba virusi vya corona vipo. Sote tuna jukumu la kupigana dhidi ya virusi hivi na kusalia salama,” akaongeza Bw Obado.

Kiongozi huyo aliwaonya wakazi dhidi ya kukongamana kwenye maeneo ya mazishi ili kuzuia uwezekano wa maambukizi mengi kuenea.

Kwa mujibu wa gavana huyo, watu hawafai kusalia kwenye ibada za mazishi kwa muda mrefu na wanafaa wahakikishe wamevalia barakoa na kuzingatia umbali wa mita moja na nusu.

“Watu wamepuuza mwongozo wa kuzuia corona kuenea. Nawaomba msisubiri maafisa wa polisi waje wawakamate kwa kupuuza mwongozo huo,” akasema.

You can share this post!

COVID-19: Visa vipya ni 404 huku wagonjwa 11 wakifariki

EACC kunasa waliopora pesa za Covid