Obiri anyakua nambari ya pili Houston Half Marathon
NA GEOFFREY ANENE
WAKENYA Hellen Obiri na Wesley Kiptoo wameridhika na nafasi za pili kwenye mbio za Houston Half Marathon nchini Amerika, Jumapili, Janauri 14, 2024.
Bingwa wa Boston na New York Marathon Obiri anayejiandaa kutetea taji la Boston Marathon hapo Aprili 15, 2024 amekamilisha mbio hizo za kilomita 21 kwa saa 1:06:07, katikati ya Waethiopia Sutume Kebede (1:04:37) na Buze Kejela (1:06:24).
Wakenya wengine katika 10-bora katika kitengo cha wanawake walikuwa Edna Kiplagat (1:07:52) na Mercy Chelangat (1:08:58) katika nafasi za sita na 10, mtawalia.
Kiptoo alikamata nafasi ya pili kwa upande wa wanaume kwa 1:00:43, akimaliza katikati ya Waethiopia Jemal Yimer (1:00:42) na Milkesa Tolosa (1:00:45).
Wakenya Peter Njeru (1:01:13) na Alex Masai (1:01:46) waliridhika na nafasi ya saba na 11, mtawalia.
Naye Vicoty Chepng’eno ameridhika na nafasi ya pili katika mbio za Houston Marathon kwa saa 2:19:55, katikati ya Waethiopia Rahma Tusa (2:19:33) na Melesech Beyene (2:24:50).
Alikuwa Mkenya wa pekee katika 10-bora upande wa kina dada.
Katika kitengo cha wanaume, Wakenya Elisha Barno na Shadrack Kimining walimaliza mbio hizo za kilomita 42 katika nafasi ya 10 na 12 kwa saa 2:14:05 na 2:14:59, mtawalia.