Habari Mseto

OCS alimuua mahabusu jela – Mahakama

December 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA mkuu wa polisi (OCS) aliyesimamia kituo cha Ruaraka kaunti ya Nairobi Alhamisi alipatiakana na hatia ya kumtesa na hatimaye kumuua muuzaji wa bidhaa katika kioski eneo la Roasters, Nairobi miaka mitano iliyopita.

Jaji Stellah Mutuku alisema Nahashon Mutua (pichani) alitumia mamlaka yake vibaya alipoamuru mhasiriwa Martin Koome azuiliwe ndani ya seli alikoteswa na kufariki masaa 20 baada ya kushikwa na kutupa korokoroni.

Jaji Mutuku alisema afisa huyo wa polisi alitumia mamlaka yake vibaya badala ya kuyatumia kudumisha usalama na kuwalinda wananchi wakiwamo mahabusu.

Koome alifia katika hospitali kuu ya Kenyatta saa 20 baada ya kuumizwa na polisi katika kituo cha polisi cha Ruaraka.

“Mshtakiwa alifanya juu chini kukwepa mkono wa sheria kwa kuwasingizia mahabusu waliokuwa wamezuliwa pamoja na Koome,” alisema Jaji Mutuku.

Mmoja wa mahabusu hao Bw Kevin Odhiambo alishikwa na kushtakiwa kwa mauaji ya Koome lakini akaachiliwa kwa kukosekana ushahidi.

“Kila mbinu zilifanywa kufunika ukweli lakini mamlaka huru ya polisi (IPOA) ilichunguza kesi hiyo na kupendekeza Mutua ashikwe na kushtakiwa.

Kiongozi wa mashtaka Mercel Ikol. Picha/ Richard Munguti

Mahakama itatoa hukumu Desemba 20 baada ya kupokea ripoti kutoka kwa afisa wa urekebishaji tabia na pia kutoka kwa jamii ya mwendazake.

Marehemu Koome , aliyekuwa na umri wa miaka 35 mnamo Desemba 20, 2013, alizuiliwa katika kituo hicho cha Polisi cha Ruaraka akiwa buheri wa afya.

“Mshtakiwa alikuwa mwenye afya nzuri alipozuiliwa katika kituo hicho cha Polisi mnamo Desemba 19, 2013,” alisema Jaji Mutuku.

Lakini Jaji huyo alisema keshoye mshtakiwa alikuwa amepigwa hadi akalemazwa kabisa na polisi.

Mahakama ilisema kuwa Koome alitiwa nguvuni baada ya majirani kupiga ripoti kwamba marehemu alikuwa na mtoto mchanga na hawajui alikuwa anampeleka wapi.

Alikamatwa na maafisa watatu wa polisi baada ya kumuona akitoka ndani ya nyumba yao akiwa na mtoto mwenye umri wa mwezi mmoja.

Alipokamatwa mkewe Peninah Kaumbuthu alimfuata hadi kituo cha polisi cha Ruaraka alipozuiliwa akiwa buheri wa afya.

Koome na Peninah walikuwa wametofautiana kinyumbani siku hiyo alipotiwa nguvuni.

Koome aliyemiliki Kiosk katika eneo la Roasters alikuwa akiishi katika mtaa wa Baba Ndogo. Nyumba yao ilikuwa mita chache kutoka kituo hicho cha Polisi.

Peninah Kaumbuthu (mwenye miwani), mkewe marehemu Martin Koome. Picha/ Richard Munguti

 

Alipofika kwa nyumba alikuwa amebeba trei ya mayai.

“Mume wangu alifika nyumba Desemba 19 2013 akiwa amebeba trei ya mayai. Alikuwa mlevi.Aliniitisha mtoto ampakate. Alitoka nje akiwa naye ndipo majirani wakakimbia kituo cha polisi na kusema mume wangu alikuwa anatoroka na mtoto,” Peninah aliambia Taifa Leo baada ya Bw Mutua kupatikana na hatia ya kumuua Koome.

Peninah ambaye hana kazi maalum amesomea kazi ya usimamizi wa mahoteli na uuzaji bidhaa.

Mshtakiwa alikuwa nje kwa dhamana.

“Tangu mume wangu auawe na Polisi nimetahabika sana kumlea mtoto wetu ambaye sasa yuko na umri wa miaka mitano.Ilibidi nirudi nyumbani kukaa na wazazi wa Koome ambao sasa ni wakongwe,” alisema Peninah.

Peninah aliyeanza kupokea vitisho baada ya kutoa ushahidi mahakamani ilibidi atoroke Nairobi.

Anaomba asaidiwe kupata kazi amsaidie mwana wao.

Mawakili wa familia walisema kuwa waliridhika haki ilitendeka na kumpongeza Jaji Mutuku kwa kutekeleza kazi yake kwa njia ya haki.