• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
OCS wa Juja adungwa mishale na wapishi wa chang’aa 

OCS wa Juja adungwa mishale na wapishi wa chang’aa 

NA MWANGI MUIRURI 

VITA vya Naibu wa Rais, Rigathi Gachagua Mlima Kenya dhidi ya pombe za mauti vimeanza kuwa hatari kwa maafisa wa kiusalama baada ya Kamanda wa kituo cha Juja kupigwa mishale kadha Jumapili jioni, Machi 31, 2024.

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi Kaunti ya Kiambu, Bw Michael Muchiri, afisa huyo kwa jina Inspekta John Misoi alikuwa ameandamana na maafisa wake katika eneo moja la maandalizi ya pombe hizo.

“Maafisa hao walikuwa katika Kijiji cha Gachororo ambapo walikuwa wamedokezewa kulikuwa na biashara ya pombe haramu na mihadarati. Afisa huyo aliongoza kikosi chake na wakakivamia,” akasema.

Bw Muchiri alisema kwamba usalama katika danguro hilo ulikuwa ‘umewekwa’ na wahuni waliokuwa wamejihami kwa vifaa butu.

“Ndipo wahuni hao walizindua mashambulizi na kwa bahati mbaya Kamanda wangu wa kituo cha Juja akajipata na mishale mwilini,” akasema.

Bw Muchiri alisema kwamba kwa sasa hawezi kufichua habari muhimu za afisa huyo kwa mujibu wa maadili ya haki ya usiri wa mgonjwa.

“Lakini cha maana kujua ni kwamba afisa huyo amelazwa katika hospitali moja Mjini Thika anakoendelea kupata matibabu, huku hali yake ikiwa ni dhabiti,” akasema Bw Muchiri.

Aliongeza kwamba shambulizi hilo halitalemaza juhudi kuhakikisha Kijiji cha Gachororo kimetiwa adabu ya kutii kukoma upishi na uuzaji wa pombe haramu, pamoja na mihadarati.

Bw Muchiri aliongeza kwamba maafisa wa ujasusi na wa uchunguzi wa makosa ya jinai wametumwa eneo hilo kunasa waliotekeleza shambulizi hilo dhidi ya afisa huyo.

  • Tags

You can share this post!

Walevi kutoka Nyeri wafurika Kirinyaga kukata kiu

Nusra Man City imuue Ndovu ikimshusha juu ya mti

T L