• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
ODM imepoteza mnato wake eneo la Pwani?

ODM imepoteza mnato wake eneo la Pwani?

Na BENSON MATHEKA

SIASA za eneo la Pwani huenda zikabadilika pakubwa baada ya kuibuka kuwa umaarufu wa chama cha ODM eneo hilo umedidimia.

Wadadisi wanasema kwamba, kimya cha vigogo wa kisiasa eneo hilo siku za hivi majuzi ni ishara kwamba linaweza kugeuza mwelekeo wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Kulingana na utafiti wa hivi punde wa kampuni ya Infotrak, umaarufu wa chama cha ODM katika eneo la Pwani umeshuka hadi asilimia 21 kutoka 50.

Wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakipigia kura chama hicho tangu 2007.

“Inaonyesha wakazi wa pwani na kwa kiwango fulani, viongozi wao wamechoka na chama hicho kwa sababu wanahisi kwamba hakiwakilishi maslahi yao kilipoamua kuunga serikali. Kumbuka kwa miaka mingi, wakazi wa pwani wamekuwa wakilalama kuwa serikali imekuwa ikiwatenga,” asema mdadisi wa siasa Ezekiel Katana.

Viongozi wa eneo hilo, akiwemo Gavana wa Mombasa Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi Amason Kingi ambao walikuwa wakikosoa serikali kabla ya kiongozi wa chama chao, Raila Odinga kusalimiana na Rais Uhuru Kenyatta, wamekuwa kimya.

Bw Joho ambaye aliunga mkono muafaka wa Odinga na Rais Kenyatta, ni naibu kiongozi wa chama cha ODM na amepunguza shughuli zake hadharani tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya handisheki.

Kulingana na Bw Katana, kumekuwa na juhudi za kuunda chama kitakachowakilisha maslahi ya wakazi wa pwani na viongozi wamekuwa wakijadiliana.

“Nafikiri kufuatia muafaka huo, viongozi wa pwani waliamua kutulia ili kujipanga bila kuanika mambo yao. Utagundua kwamba siku hizi hata wabunge wa eneo hilo waliokuwa wakiunga viongozi wa kitaifa wametuliza boli,” asema.

Wabunge kadhaa wa eneo hilo, akiwemo Owen Baya(Kilifi North) Paul Katana(Kaloleni) Khatib Mwashetani (LungaLunga), Aisha Jumwa (Malindi) na Suleiman Dori (Mswambweni) ambao walikuwa wakimuunga Naibu Rais William Ruto wamepunguza mikutano ya hadhara.

Wakati wa sherehe za Madaraka mwaka 2019, agavana Joho, Kingi na mwenzao wa Kwale Salim Mvurya walihimizwa kuungana kabla ya 2022.

“Wakati umefika sisi kama Wapwani kuamua mwelekeo wetu wa kisiasa na tunaweza kufanya hivi kwa kuungana,” alisema mbunge wa Kisauni Ali Mbogo.

‘Chungwa limeisha ladha’

Bw Katana anasema kwamba, kufuatia matukio ya kisiasa nchini, wakazi wa pwani wanahisi kwamba upinzani hauwafai na hii ndiyo imefanya umaarufu wa ODM kupungua eneo hilo.

Utafiti wa Infortrack ulionyesha kuwa asilimia 56 ya wakazi wa pwani wanahisi kwamba upinzani hautekelezi majukumu yake.

“Hii ni sawa na kufahamisha viongozi wa ODM kwamba wanataka mabadiliko na wameamua kufanya sasa,” aeleza Bw Katana.

Mbunge mmoja wa ODM ambaye hakutaka tutaje jina lake kwa sababu ya uhusiano wake na viongozi wa chama hicho alisema wakazi wa pwani wanahisi chama hicho huwa kinawatumia tu wakati wa kura na kisha kuwatelekeza.

Anatoa mfano wa Kaunti ya Kilifi ambapo ni madiwani watatu pekee ambao sio wa chama hicho mbali ODM hakijarudisha mkono kwa wakazi licha ya Odinga kuunga serikali.

  • Tags

You can share this post!

Ruhusa yatoka magunia 12m ya mahindi yaagizwe

Demu akataa kuishi na wakwe kijijini

adminleo