Habari Mseto

ODM yamtetea Raila kuhusu sakata ya dhahabu

May 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha ODM kimekana madai kuwa kiongozi wake alihusika katika sakata ya uuzaji wa dhahabu feki ambapo inadaiwa kuwa Mwanamfalme wa Milki za Kiarabu (UAE) Sheik Mohammed bin Rashid al Maktoum alitapeliwa Sh400 milioni na walaghai kutoka Kenya.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho Philip Etale na Mkurugenzi wa Masuala ya Kisiasa Opiyo Wandayi, Jumamosi walipuuzilia mbali hatua ya viongozi wa Jubilee, wanaoegemea mrengo wa Naibu Rais William Ruto, kumhusisha Bw Odinga na sakata hiyo.

“Wanaotoa madai hayo wanaendeleza ajenda ya kisiasa ambayo haihusiani na uchunguzi unaoendelea. Bw Odinga hahusiki kwa njia yoyote katika sakata hiyo,” akasema Bw Etale.

Naye Bw Wandayi ambaye pia ni Mbunge wa Ugunja aliwataka Gavana Ferdinand Waititu na wandani wa Dkt Ruto waliomtaka Bw Odinga kuelezea anachofahamu kuhusu sakata hiyo kusubiri kukamilishwa kwa uchunguzi unaoendelea.

“Waititu na wenzake hawafai kuingilia uchunguzi unaoendelea kwa kuanza kutaja jina la kiongozi wa chama chetu. Hii ni sawa na kuingiza siasa katika sakata hii ambayo bado inachunguzwa licha ya washukiwa kadhaa kufikishwa kortini majuzi,” akasema.

Raila atakiwa kutoa maelezo

Jumamosi, Bw Waititu aliwaongozwa wabunge wengine wa Jubilee kumtaka Bw Odinga kuelezea anachofahamu kuhusu sakata hiyo.

“Inasikitisha kuwa Bw Odinga amekuwa akihusisha viongozi wengine na ufisadi ilhali yeye ndiye amekuwa mstari wa mbele kuwatapeli watu wengine pesa zao. Raila na wahusika wengine sharti walazimishwe kurejesha fedha walizopata katika sakata hiyo,” akasema katika maeneobunge ya Endebess na Saboti.

Wabunge wengine walioandamana na Dkt Ruto katika ziara hiyo pia waliunga mkono kauli ya Bw Waititu.