• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
ODM yataka hoteli ya Ruto ibomolewe

ODM yataka hoteli ya Ruto ibomolewe

Na GITONGA MARETE

VIONGOZI wa chama cha ODM, sasa wanataka Hoteli ya Weston inayomilikiwa na Naibu wa Rais William Ruto ibomolewe, na ardhi hiyo irudishiwe Mamlaka ya Safari za Angani (KCAA).

Tume ya Ardhi (NLC), mapema mwezi huu iliamua kuwa ardhi ambapo hoteli hiyo imejengwa ilinyakuliwa, hivyo, Dkt Ruto anafaa kulipa fidia kwa mamlaka ya KCAA.

Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, aliyekuwa akizungumza katika eneo la Nkubu, Kaunti ya Meru, alisema sheria inafaa kutumika kubomoa hoteli ya Weston bila kujali wadhifa ambao mmiliki wake anashikilia serikalini.

“Majumba yaliyojengwa katika hifadhi za barabara au kando ya vyanzo vya maji yamebomolewa. Mbona Hoteli ya Weston imeachwa? Tunataka hoteli hiyo ibomolewe na ardhi ikabidhiwe kwa mmiliki wake ambaye ni mamlaka ya KCAA,” akasema Bw Sifuna aliyekuwa ameandamana na naibu wake Dkt Agnes Zani na viongozi wa ODM tawi la Meru.

“Naibu wa Rais mwenyewe alikiri kuwa kipande hicho cha ardhi kilinyakuliwa, hiyo inamaanisha kuwa kinafaa kurejeshwa kwa mmiliki wake halali. Mamlaka ya KCAA haifai kulipwa fidia kwa sababu haitapata kipande sawa na hicho katika eneo hilo,” akaongezea.

Alisema vita dhidi ya ufisadi ni miongoni mwa masuala ambayo Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga waliafikiana kabla ya kutangaza kushirikiana.

“Hatuwezi kuzungumzia mwafaka wa ushirikiano baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga bila kuzungumzia ufisadi. Rais Kenyatta na Bw Odinga wamejitokeza na kukemea vikali ufisadi,” akasema.

You can share this post!

Shinikizo Amina ajiuzulu kuhusu mikopo ya HELB

Kenya njia panda kuhusu mizozo na majirani wake

adminleo