Ojaamong alichaguliwa kihalali, Odima alipe Sh12 milioni, Mahakama yaamuru
Na CECIL ODONGO
Kwa Muhtsari:
- Kesi hiyo iliyokuwa imewasilishwa kortini na Bw Peter Odima Khasamula ilifutwa kwa kukosa kuthibitisha kwamba Bw Ojamoong alitumia njia zisizofaa kuibuka mshindi
- Mlalamishi atakiwa aigaramie kesi hiyo kwa kuwalipa IEBC na Gavana Ojaamong jumla ya Sh12 millioni
- Ojaamong sasa ana fursa ya kuanzisha na kuimaliza miradi aliyowaahidi wakazi wa kaunti hiyo
GAVANA wa Busia Sospeter Ojaamong aliponea Jumatatu kupoteza wadhifa wake mahakama ya Busia ilipohalalisha ushindi wake na kutupilia mbali kesi ya uchaguzi iliyokuwa ikimwandama.
Jaji Kiarie Waweru alitupilia mbali kesi hiyo iliyokuwa imewasilishwa kortini na Bw Peter Odima Khasamula akisema alikosa kuthibitishia korti kwamba Bw Ojamoong alitumia njia zisizofaa kushinda kura.
Bw Odima alikuwa meneja wa kampeni ya aliyekuwa mbunge wa funyula Dkt Paul Otuoma, mpinzani wa gavana aliyeibuka wa pili kwenye uchaguzi huo.
Sh12 milioni
Kulingana na uamuzi uliotolewa na jaji, mlalamishi huyo alitakiwa aigaramie kesi hiyo kwa kuwalipa IEBC na Gavana Ojaamong jumla ya Sh12 millioni.
Gavana huyo aliyehudumu kwa muda wa miaka kumi kama mbunge wa iliyokuwa eneo bunge la Teso amekuwa na uhasama mkali wa kisiasa na Bw Otuoma. Eneo bunge hilo liligawanywa na kwa sasa ni Teso kusini na Teso kaskazini.
Mashindano makali ya kisiasa kati ya wawili hao yalifikia kilele mapema mwaka jana wakati wa mchujo wa kupigania mpeperushaji tiketi ya chama cha ODM. Walilaumiana kila moja akishikilia kuwa mshindi kwenye mchujo huo.
Wizi wa kura
Bw Otuoma aliyemlaumu gavana kwa kumuibia kura aliamua kukigura chama na kuwania wadhifa huo kama mgombezi huru. Alishindwa kwa kura 125,905 dhidi ya 135153 zake Bw Ojaamong.
Ufuasi mkubwa wa chama cha ODM kaunti hiyo umetajwa na wadadisi wengi kama kisababishi kikuu cha kushindwa kwa Bw Otuoma licha ya asilimia kubwa ya jamii ya Waluhya anakotoka kuwa wenyeji wa kaunti hiyo, kujitokeza kupiga kura.
Kumalizika kwa kesi hiyo sasa kunampa gavana huyo fursa ya kukamilisha kipindi chake cha pili na kuanzisha na kumaliza miradi aliyowaahidi wakazi wa kaunti hiyo.