Omtatah afika mahakamani kupinga sare za buluu
Na RICHARD MUNGUTI
MWANAHARAKATI Okiya Omtatah Ijumaa aliwasilisha kesi kupinga mabadiliko katika Idara ya Polisi yaliyotangazwa Alhamisi na Rais Uhuru Kenyatta ikiwa ni pamoja na kuzinduliwa kwa mavazi ya rangi ya samawati.
Katika kesi aliyowasilisha chini ya sheria za dharura, Bw Omtatah amesema endapo mahakama haitasitisha kutekelezwa kwa mageuzi hayo bila shaka haki za wananchi zitakuwa zimekandamizwa.
Bw Omtatah anasema katika kesi hiyo kwamba Rais Kenyatta alikaidi Katiba kwa kujaribu kutangaza mabadiliko katika muundo msingi wa kikosi cha Polisi kama inavyoamriwa katika Vifungu vya Katiba vinavyoeleza jinsi Rais anaweza kutumia mamlaka yake.
Bw Omtata anasema kuwa Vikosi vya Polisi wa kawaida na Polisi wa Utawala vimebuniwa kwa mujibu wa katiba na kazi zinazotekelezwa na vikosi hivi.
Mtetezi huyu wa haki za binadamu ameeleza katika kesi aliyoomba isikizwe wakati huu wa likizo ya Agosti ya Majaji wa mahakama kuu kwamba “endapo korti haitaingilia kati na kusitisha kitekelezwa kwa mageuzi hayo katika utenda kazi na muundo msingi na usimamizi wa vikosi vya Polisi wa Utawala , GSU na Polisi wa kawaida huenda haki za wananchi zikakandamizwa.”
Mnamo Septemba 13, 2018 Rais Kenyatta alitangaza mabadiliko makubwa katika kikosi cha Polisi ambapo aliunganisha vikosi vya Polisi wa Utawala na Polisi wa kawaida.
Mahakama imeelezwa kuwa baadhi ya vyeo katika kikosi cha polisi vimefutuliwa mbali .
“Kazi zinazotekelezwa na vikosi hivi vya polisi imeelezewa kinanga ubaga kwenye katiba na pia katika sheria za Polisi,” anasema Bw Omtatah katika kesi aliyosema ikon a umuhimu mkubwa kwa umma.
Katika kesi hiyo Bw Omtatah amewashtaki Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’I na mwanasheria mkuu (AG) Paula Kihara Kariuki.
Katika kesi hiyo Bw Omtatah alisema makamanda wa polisi wanaosimamia vituo au maeneo wameondolewa.
Pia amesema kuwa maafisa wa Polisi wav yeo vya chini watakuwa wanapewa pesa za kukodisha nyumba pamoja na wananchi wanaowalinda.
Bw Omtatah anasema katika kesi aliyoiwasilisha siku moja baada ya Rais Kenyatta kutangaza mabadiliko hayo, kuwa haijacheleweshwa kwa vile aliishtaki kwa pupa inayostahili.