Habari Mseto

Omtatah aingia mitandaoni kuelezea furaha yake kukomboa kipande cha ardhi

August 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

MWANAHARAKATI Okiya Omtatah, amevutia nyoyo za Wakenya baada ya kukomboa ekari 843 za ardhi ya umma iliyonyakuliwa kupitia kesi iliyomchukua miaka minane na nusu.

Bw Omtatah alijitosa mitandaoni Ijumaa kufichua kufaulu kwake katika kesi aliyowasilisha mnamo 2012, dhidi ya Kiwanda cha Sukari Busia (BSC), akitaka kipande cha ardhi ya serikali kilichonyakuliwa Nasewa, eneobunge la Matayos, Kaunti ya Busia, kurejeshewa wananchi.

“Baada ya miaka minane na nusu ya kutetea na kuwasilisha kesi, niliokoa kipande cha ardhi ya serikali ya ekari 843 katika kaunti ya Busia kutoka kwa matapeli waliokuwa wameinyakua na nikakirejesha kwa umma,” aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.

Aidha, mwanaharati huyo alifichua kwamba Msajili wa Ardhi Kaunti ya Busia, alifutilia mbali cheti cha kumiliki ardhi kilichotolewa kwa njia haramu kwa kampuni ya kibinafsi ya BSC, na kutoa cheti kipya kwa jina la Katibu Mkuu, Hazina ya Kitaifa, ambaye ndiye anayesimamia mali yote ya Serikali ya Kitaifa.

Bw Omtatah aliikabidhi serikali cheti hicho kipya kupitia Kamishna wa Kaunti ya Busia.

“Niliikabidhi Serikali cheti kipya cha ardhi kupitia Kamishna wa Kaunti Busia. Cheti hicho kimetumwa kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi atakayekihifadhi kwa niaba ya Wakenya,” alisema.

Katika kesi yake, Bw Omtatah aliitaka mahakama kufutilia mbali kutengwa kwa aina yoyote, kuhamishwa kwa ardhi kwa BSC au kampuni ya Kaplony, maadamu kila kitu kilifanywa kinyume na sheria.

Mahakama ya Mazingira na Ardhi Bungoma, mnamo Julai 31,2018, ilitupilia mbali cheti cha umilisi cha BSC, huku uamuzi wa mahakama ukisema, haikufaa kwa ardhi hiyo iliyopatiwa wakazi, kupatiwa kampuni za kibinafsi kwa matumizi yao binafsi.

Isitoshe, jaji aliitangaza BSC kuwa shirika la kibinafsi huku wenyehisa wakiwa serikali, mwakilishi wa kampuni ya Booker Tate nchini, MH Da Gama Rose, na kampuni ya Reliant Holdings.

Wakenya walijitosa mitandaoni kumpongeza Bw Omtatah, huku wakimwita shujaa, na kusema kwamba ilikuwa wazi kwamba si lazima uchaguliwe katika afisi fulani ili uhudumie wananchi na taifa.