Habari Mseto

Omtatah apeleka kesi kortini akitaka Maraga atimuliwe

March 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAHARAKATI na mtetezi wa haki za binadamu Okiya Omtatah amewasilisha ombi la kumtimua Jaji Mkuu David Maraga kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Katika ombi alilowasilisha mbele ya Tume ya kuajiri watumishi wa Idara ya Mahakama (JSC), Bw Omtatah alidai kuwa Jaji Maraga alivuruga kesi aliyowasilisha mahakamani kuhusu harakati ya kujaza pengo la Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bw Edward Ouko.

Bw Omtatah alighadhabishwa na hatua ya Jaji Maraga kuitisha faili ya kesi hiyo na kutoa maagizo kabla ya uamuzi kutolewa.

Mwanaharakati huyo anadai kuwa hatua ya Jaji Mkuu kusimamisha kusomwa kwa uamuzi kuhusu kesi ya kuteuliwa kwa mkaguzi mkuu mpya ufuatia kustaafu kwa Bw Ouko, ilikuwa sawa na kuingilia uhuru wa mahakama kuu.

Bw Omtatah alisema katika kesi hiyo kwamba tabia hiyo ya Jaji Maraga aliye pia Rais wa mahakama ya juu, haiambatani na mwenendo wa jaji na ni kinyume cha kiapo chake cha kulinda katiba na kuitetea.

Bw Omtatah anadai kuwa Jaji Maraga aliitisha faili ya kesi hiyo na kusitisha kwa muda usiojulikana utoaji na usomaji wa uamuzi wa kesi aliyowasilisha.

Kesi hiyo ilisikizwa na Jaji Stephen Radido wa mahakama ya kuamuzi mizozo ya ajira (ELRC).

Bado Jaji Maraga hajajibu kesi hiyo iliyowasilishwa mbele ya JSC ambapo ndiye mwenyekiti wake.

Katika kesi aliyowasilisha kuhusu ajira ya atakayetwaa wadhifa wa mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali, Bw Omtatah alipinga hatua ya Serikali ya kutangaza upya wadhifa huo kufuatia kustaafu kwa Bw Ouko mwaka 2019.

Jaji Radido alikuwa ametenga Februari 26, 2020 kama siku ya kutoa uamuzi kuhusu ujazaji wa pengo hilo.