Omtatah atuzwa tena
Na CHARLES WASONGA
MWANAHARAKATI Okiya Omtatah Okoiti Jumamosi alitunukiwa tuzo ya heshima kutokana na juhudi zake za kupigania haki za kibinadamu kwa ajili ya kuboresha jamii.
Alipokezwa tuzo hiyo kwa jina “2020 Heroes Award” na Raphael Obonyo, mkurugenzi mkuu wa wakfu wa “Foundation Award”, katika hafla fupi iliyofanyika Nairobi na kuhudhuriwa na watu wachache walioalikwa pekee.
Wakfu huo huwatuza watu waliojitolea kutetea haki na masilahi ya kijamii kwa ujasiri kila mwaka.
Bw Obonyo ambaye ni Mshauri wa Umoja wa Kimataifa (UN) na kiongozi wa vuguvugu la Youth Congress, alisema kuwa tuzo hiyo spesheli hupewa watu waliojitolea mhanga kuleta matumaini kwa wanajamii.
“Ujasiri na kujitolea kwa Omtatah katika kupigania haki za kibinadamu ni sifa ambayo sote tunapaswa kuiga,” akasema.
Akipokea tuzo hiyo, mwanaharakati huyo alisema amepata nguvu na moyo na tuzo hiyo na kuahidi kuendelea kupigania haki za wanaonyanyaswa katika jamii.
“Asante kwa heshima hii. Nimeipokea kwa moyo mkunjufu na inanipa moyo kuendelea kutetea haki za raia. Nashukuru zaidi,” akasema Omtatah.
Akaongeza: “Kwangu wajibu mkubwa wa kuishi ni kuwahudumia wanadamu. Sidhani msukumo wa maisha ni kujilimbikizia mali. Muhimu ni kuishi maisha ya kawaida, kuwa na tabia nzuri na kuwatumikia wananch kwa njia bora na inayoridhisha.”
Mwanaharakati huyo ameshinda kesi nyingi mahakamani, kesi ambazo zinahusu masilahi ya umma.
Miongoni mwa tuzo ambazo amepokea ni; “Lifetime Achievement Award,” kutoka kwa mashirika ya National Coalition of Human Rights Defender,” na “Working Group on Human Defenders”.
Mnamo Machi 2020, Bw Omtata aliwasilisha ombi katika Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) akitaka Jaji Mkuu anayeondoka David Maraga achunguzwe kwa madai ya kushiriki mienendo mibaya.
Alimsuta Maraga kwa kuingilia uhuru wa jaji mmoja katika kesi ambayo aliwasilisha katika mahakama kupinga hatua ya serikali kutangaza kiti cha mkaguzi wa hesabu za serikali kuwa wazi akiwataka waliohitimu kutuma maombi ya kujaza nafasi hiyo.
Mnamo Juni Bw Omtatah alifaulu kushawishi jopo la majaji watatu; Martha Koome, Gatembu Kairu na Jamila Mohammed kwamba Shirika la Reli Nchini (KR) lilifeli kuzingatia sheria za ununuzi wa bidhaa za umma lilipotoa zabuni ya ujenzi wa reli ya kisasa, SGR.
Mahakama ya Rufaa iliamua kwamba kandarasi ya mradi huo mkubwa wa miundomsingi ilitolewa kinyume cha sheria.