Habari Mseto

Ongezeko la bangi Bonde la Ufa linavyofanya maafisa wa usalama kukuna vichwa

February 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

VITALIS KIMUTAI NA WANDERI KAMAU

ULANGUZI na uuzaji haramu wa bangi umegeuka kuwa donda sugu katika eneo la Kusini mwa Bonde la Ufa, licha ya msako ambao umekuwa ukiendeshwa na idara kadhaa za serikali.

Vijana wamejiingiza katika biashara hiyo haramu, inayoendelea kushika kasi katika kaunti za Bomet, Kericho, Narok na Nakuru.

Pia, imeibainika kuwa bangi imekuwa ikiingizwa nchini kiharamu kutoka nchi jirani za Tanzania na Uganda, kwenye mtandao wa kibiashara wa mipakani wenye thamani ya mamilioni ya pesa.

Mnamo Jumanne wiki iliyopita, Kamishna wa Kaunti ya Bomet Dkt Mohamed Omar na Kamanda wa Polisi wa Kaunti, Bw Robinson Ndiwa, waliwaongoza polisi kuchoma bangi yenye thamani ya Sh2 milioni.

Ni hali iliyotajwa kuonyesha jinsi biashara ya ulanguzi wa mihadarati imekithiri katika eneo la Kusini mwa Bonde la Ufa.

Uchomaji wa bangi hiyo ulifanyika kwenye jaa la kutupia taka la Bomet, na ulifuatia maagizo ya mahakama yaliyotolewa kwa polisi.

Bangi hiyo, iliyokuwa kwenye magunia sita, ilinaswa kwenye visa tofauti katika eneo hilo kwa muda wa miaka mitatu iliyopita.

“Wafanyabishara walaghai wamekuwa wakitumia barabara ya Isibania-Kisii-Sotik-Narok kusafirisha mihadarati hiyo. Sehemu yake imekuwa ikiuzwa katika baadhi ya maeneo ya Bonde la Ufa huku inayobaki ikisafirishwa hadi jijini Nairobi,” akasema Dkt Omar.

Kamishna huyo alisema kuwa wauzaji wamekuwa wakitumia magari ya uchukuzi wa umma, ya kifahari na yale madogo madogo kusafirisha bidhaa hiyo, ili kutonaswa na polisi.

“Polisi wa trafiki wamekuwa tu wakiyalenga magari ya uchukuzi wa umma na Toyota Probox. Hata hivyo, imeibuka kuwa walanguzi wanatumia magari ya kifahari ya kibinafsi kuisafirisha,” akasema.

Bw Ndiwa, naye alisema kuwa kwa ushirikiano na umma, polisi wamefanikiwa kuwakamata wauzaji kadhaa, baada ya kupokea habari za kijasusi.

Kwenye njia ya kukwepa mitego ya polisi, walanguzi hao wamekuwa wakitumia barabara za vichochoro ambako polisi huwa hawaweki vizuizi vya barabarani.

“Kaunti zilizo katika maeneo ya Magharibi na Nyanza huwa zinatumiwa sana kuingiza bidhaa hiyo kutoka nchi jirani,” akasema polisi anayehusika kwenye uchunguzi kuhusu biashara hiyo.