Onyo kali kwa wanabodaboda Lamu
NA KALUME KAZUNGU
SERIKALI ya Kaunti ya Lamu imewataka wahudmu wa boda boda kisiwani Lamu kuheshimu sheria inayowazuia kuhudumu ndani ya mji wa Shella.
Waziri wa Utalii, Biashara na Viwanda wa Kaunti ya Lamu, Dismas Mwasambu, anasema sheria hiyo imejumuishwa na ile iliyowekwa hivi majuzi ya kuwataka kutohudumu ndani ya mji wa kale wa Lamu.
Jumatatu waendeshaji pikipiki zaidi ya 100 waliandamana na kuziba barabara ya Lamu kuelekea Shella katika eneo la Duduvilla kupinga kile walichodai kuwa ni unyanyasaji na ukandamizaji wa baadhi ya wakuu wa usalama wa kaunti ya Lamu.
Wahudumu hao wa boda boda waliwakashifu wakuu hao wa usalama kwa kuwazuia kuhudumu kwenye mji wa Shella na kutaja hatua hiyo kuwa yenye lengo la kusambaratisha biashara yao.
Katika mahojiano na Taifa Leo Ijumaa aidha, Bw Mwasambu alishikilia kuwa Shella ni miongoni mwa miji ya Lamu ambayo hupokea wageni wengi hasa watalii kila mwaka ambao huvutiwa na ukale wa mji huo.
Alisema mbali na kuhifadhi ukale na historia ya mji wa Lamu, idara yake imeandaa mikakati kabambe ya kuhakikisha miji mingine ya kihistoria kote Lamu inahifadhiwa.
Aliwataka wahudumu hao wa boda boda kuheshimu sheria hiyo la sivyo wakamatwe na kushtakiwa.
“Wasiseme sheria hiyo imewekwa katika mji wa kale wa Lamu pekee. Hapana. Sheria hiyo inafanya kazi hata Shella. Hakuna pikipiki zitakazoruhusiwa kuendeshwa ndani ya mji wa Shella. Huo ni mji unaopokea wageni wengi wanaovutiwa na historia na ukale wake. Wahudumu wa boda boda wanaruhusiwa tu kuendesha pikipiki zao nje ya mji huo na wala si ndani ya mji,” akasema Bw Mwasambu.
Kufuatia sheria hiyo, wahudumu wa pikipiki watahitajika kuendesha pikipiki zao kwenye barabara za nje ya Shella hadi nje ya Lamu, nje ya Lamu hadi mitaa ya Kashmir, Bombay, Kandahar, Mararani, Wiyoni na sehemu zingine zilizoko viungani mwa miji hiyo miwili mikuu.
Mnamo Agosti 2015, serikali ya kaunti ya Lamu iliafikia kupiga marufuku uendeshaji wa pikipiki, magari na baiskeli ndani ya kisiwa cha Lamu kama njia mojawapo ya kuhifadhi ukale na historia ya mji huo.
Usafiri ulioruhusiwa ulikuwa ule wa miguu na punda pekee.
Aidha kati ya 2017 na 2018, wahudumu wa pikipiki walianza kurudi na kutekeleza shughuli zao ndani ya kisiwa cha Lamu.
Kufikia sasa zaidi ya pikipiki 150 zinaendeshwa ndani ya kisiwa cha Lamu, hatua ambayo ni kinyume cha sheria zinazoambatana na ukale wa mji huo.
Mnamo 2001, mji wa kale wa Lamu uliorodheshwa na Shirika la Kisayansi, Elimu na Utamaduni ulimwenguni (UNESCO) kama eneo mojawapo linalotambulika zaidi kwa kuhifadhi tamaduni na ukale wake, yaani-UNESCO World Heritage Site.