Habari Mseto

Onyo kali kwa wanaokeketa wasichana kisiri

February 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na PAULINE ONGAJI

[email protected]

Katibu Mkuu wa Usimamizi katika Wizara ya Utumishi wa Umma na Jinsia Bi Rachel Shebesh ametoa onyo kali kwa wale wanaoendelea kutekeleza ukeketaji katika sehemu mbalimbali nchini kisiri.

Alisema haya wakati katika majadiliano na kikundi cha vijana wanaoendeleza vita dhidi ya ukeketaji katika sehemu mbalimbali nchini, shughuli iliyoandaliwa katika Kanisa Katoliki la St Eusabius, katika Kaunti ya Isiolo.

Katika hafla hiyo ambapo alitoa nakala sahili za makosa chini ya Sheria ya Kupambana na Ukeketaji Mwaka 2011, Bi Shebesh alisema kwamba wanaoendelea kutekeleza uovu huu wanakumbwa na hatari ya kuhudumu kifungo na adhabu kali endapo watapatikana na makosa.

Japo alisema kwamba utamaduni barani Afrika kama sehemu zingine ni muhimu, alieleza kuwa itikadi mbaya zinapaswa kukomeshwa.

“Kama wavulana kutoka sehemu zinazotekeleza utamaduni huu mnapaswa kuoa wasichana ambao hawajatahiriwa na wakati huo huo kuwa na fahari ya kufanya hivyo. Mnapaswa kufunza mbinu mbadala za kitamaduni pasi na kuathiri ujinsia na uke wa watoto wasichana .”

Akizungumza katika hafla hiyo hiyo, Mwakilishi wa Hazina ya Umoja wa Mataifa inayohusika na idadi ya watu – UNFPA nchini Dkt Ademola Olajide alisema kwamba wakati umetimia kwa utamaduni wa kukeketa wasichana kuangamizwa kabisa.

“Hiki ni kizazi ambacho kitashuhudia mwisho wa ukeketaji,” aliongeza.

Hafla hii ilikuwa mojawapo ya mikutano ya maandalizi kabla ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kuungamiza ukeketaji inayotarajiwa kufanyika hapo kesho katika Kaunti ya Isiolo.