Habari Mseto

Oparanya apigania mabadiliko ya kuupa nguvu ugatuzi

October 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SHABAN MAKOKHA

BARAZA la Magavana Nchini (COG) limeshikilia kwamba mabadiliko ya katiba yanayopendekezwa yanafaa kutilia maanani kutoa nguvu zaidi kwa mfumo wa utawala wa ugatuzi.

Mwenyekiti wa baraza hilo Wycliffe Oparanya, alisema ugatuzi umebadilisha pakubwa maisha ya Wakenya tangu uanze kutekelezwa 2013, na hivyo viongozi na Wakenya wanafaa kujadili namna ya kuhakikisha ugatuzi unatelelezwa kikamilifu.

“Leo watu wa Kakamega wanafurahia matunda ya ugatuzi kupitia miradi mbalimbali ambayo haikuwepo hapo awali. Kwa kifupi ugatuzi una manufaa mengi kwa raia iwapo utatekelezwa kikamilifu,” akasema Bw Oparanya wakati wa sherehe za Mashujaa katika uwanja wa shule ya msingi ya Muslim, eneobunge la Navakholo.

Licha ya kusifu manafaa ya ugatuzi, Bw Oparanya alidai kwamba kuna watu wachache ambao wana nia ya kusambaratisha serikali za kaunti na kutokomeza ufanisi ambao umepatikana.

Alisisitiza kwamba marekebisho ya katiba lazima yatekelezwe kuhakikisha kuna usawa wa ugavi wa mapato ya nchi na pia kuimarisha umoja kati ya Wakenya.

Vilevile alisema mabadiliko hayo yanafaa kuhakikisha mabunge ya kaunti yanafanya kazi bila kuingiliwa na pia hazina ya maendeleo ya wadi inabuniwa ili madiwani wapate fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Hazina ya maendeleo ya wadi inafaa kujumuisha asilimia 30 za bajeti ya maendeleo inayotengewa kaunti,” akaongeza Bw Oparanya.

Gavana huyo ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Chama cha ODM, alisema mabadiliko hayo yanafaa kujumuisha mapendekezo ya Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) kwamba kiwango cha fedha kinachotengewa serikali za kaunti hakifai kupungua kwa asilimia tatu ikilinganishwa na kile kinachotolewa na tume hiyo.

Ufanikishaji

Pia alisisitiza kwamba vuguvugu la Ugatuzi ambalo lilibuniwa majuzi linazingatia njia za kuhakikisha ugatuzi unafanikiwa.

“Tutazindua kampeni za kitaifa za Vuguvugu la Ugatuzi ili kuwaeleza Wakenya ukweli kuhusu serikali za kaunti na namna ya kuziimarisha,” akasema.

Alisema mapendekezo ya vuguvugu hilo yanatokana na changamoto ambazo huwakabili magavana kwenye utendakazi wao tangu mfumo huo wa utawala uasisiwe.

Kaunti zimekuwa zikikabiliwa na wakati mgumu kutokana na uhasama kati ya Mabunge ya Kitaifa na Seneti.