Pasta aliyeingia afisi ya Matiang'i bila idhini ahukumiwa
Na Richard Munguti
MHUBURI aliyeshtakiwa kuhatarisha amani kwa kuingia katika Afisi ya Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i alihukumiwa Jumanne kifungo cha nje cha mwaka mmoja.
Bi Jemimah Wangari Waruingi (pichani) aliyejitetea kuwa alikuwa akitaka Dkt Matiang’i ampeleke kwa Jaji Mkuu David Maraga amsaidie kuamua kesi ya shamba atakuwa anaripoti kwa maafisa wa urekebishaji tabia Bw Peter Macharia na Bi Jenevive Akinyi.
Wakati wa kipindi hicho, Bi Waruingi atakuwa akipokea mashauri ya kiroho pamoja na kupewa wakili wa Serikali atakayemsaidia kutatua mzozo wa shamba lao.
Bi Waruingi alitiwa nguvuni Juni 25 baada ya kupiga kambi nje ya Afisi ya Rais tangu Alhamisi wiki iliyopita akitaka akubaliwe amwone Dkt Matiang’i.
Bi Waruingi alishtakiwa kuwa mnamo Juni 25 2018 alihatarisha amani kwa kusema “Lazima nimwone Matiang’i, lazima shida yangu ijulikane leo.” Mshtakiwa huyo alikiri alihatarisha amani alipowashurutisha maafisa wa usalama wanaolinda jumba lililo na Afisi ya Rais wamkubalie amwone Dkt Matiang’i.
Kiongozi wa mashtaka alimweleza hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot kuwa mshtakiwa alikusanya umati mkubwa wa wananchi alioanza kuwahubiria na kutumia lugha ya kuhatarisha amani.
Mshtakiwa alidai aliendeleza ibada nje ya afisi ya Dkt Matiang’i kwa mujibu wa ujumbe aliopewa na Mungu kuhusu nchi hii.
Alisema kuwa sio mara yake ya kwanza kuhubiri nje ya afisi ya Rais na hata katika Ikulu ya Nairobi.
“Niliwahi kufurushwa nje ya Ikulu ya Nairobi nilipompelekea ujumbe Rais mstaafu Mwai Kibaki kwamba nchi hii itakuwa na umwagikaji wa damu kabla ya mwaka wa 2007,” alisema mshtakiwa.
Pia aliambia hakimu kuwa ilibidi afike katika afisi ya Dkt Matiang’i kwa vile kesi ya shamba la baba yake marehemu Muturi Ndirangu imekwama katika mahakama ya Nakuru na yeye pamoja na ndugu zake wanaendelea kuumia.
“Niliwasilisha kesi niteuliwe kuwa msimamizi wa mali ya baba yangu inayojumuisha mashamba katika kaunti ya Nakuru. Nilipewa barua za muda kisha kesi ikahamishwa kutoka Nairobi hadi Nakuru,” alisema Bi Waruingi.
Aliambia korti kesi hiyo haijaendelea katika mahakama ya Nakuru na aliona ni heri atafute msaada wa Dkt Matiang’i ampeleke kwa Jaji Maraga kesi yao iamuliwe mara moja.
“Je, uko na stakabadhi yoyote kuonyesha uko na kesi Nakuru,” Bw Cheruiyot alimuuliza mshtakiwa.
“Ndio,” akajibu mshtakiwa na kusema faili ya kesi iko nyumbani kwanke mtaani Kayole.
Mwishowe, mshtakiwa alishukuru alipopewa maagizo na korti. “Maneno yangu yamefika kule nilinuia.”