Habari Mseto

Pasta anayedaiwa kulaghai vijana mamilioni aachiliwa

March 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA TITUS OMINDE

MCHUNGAJI mwenye umri wa miaka 65 ambaye pia ni mwalimu mkuu mstaafu wa shule ya upili anayekabiliwa na mashtaka 48 ya kulaghai vijana mamilioni ya pesa kwa ahadi ya kuwasaidia kupata ajira katika jeshi la Uingereza ameachiliwa kwa bondi ya Sh2.2 milioni baada ya kukana mashtaka.

Kasisi Dinah Jepchumba ambaye amekuwa kwenye mtandao wa polisi kwa zaidi ya mwaka mmoja alikuwa amenyimwa dhamana wiki tatu zilizopita lakini siku ya Ijumaa mahakama ya Eldoret ilimwachilia kwa bondi ya sh2,250,000 baada ya ripoti ya maafisa wa kurekebisha tabia iliyowasilishwa kortini kumpendelea.

Bi Jepchumba alikuwa ameshtakiwa mbele ya hakimu mkuu Dennis Mikoyan kwa mashtaka 48 ya kujipatia pesa kwa njia za uwongo kinyume na kifungu cha 313 cha kanuni ya adhabu.

Mwendesha mashtaka aliambia mahakama kwamba alipata pesa hizo kutoka kwa vijana 48 wasio na ajira kutoka Uasin Gishu na kaunti jirani kwa ahadi ya kuwasaidia kupata kazi za mishahara minono katika jeshi la Uingereza.

Kulingana na faili 48 za mashtaka mahakamani, alidaiwa kupata kiwango cha juu cha Sh150,000 kutoka kwa kila mwathiriwa ambapo kwa jumla alijipatia zaidi ya Sh5 milioni.

Waathiriwa waliambia maafisa wa uchunguzi kutoka kituo cha polisi cha Naiberi kuwa walikuwa wakilipa kati ya Sh40,000 na Sh150,000 kulingana na hali ya kazi waliyoahidiwa.

Wakili wa serikali Jamlek Muriithi aliambia mahakama kuwa mshtakiwa alipata pesa hizo kutoka kwa vijana walio katika mazingira magumu kwa tarehe tofauti kati ya Juni na Julai 2023.

Kesi hiyo itatajwa Machi14, kabla ya kupewa siku ya kusikizwa.