Pasta taabani kumlaghai Mjapani Sh1.2 milioni za kueneza injili
Na DENNIS LUBANGA
POLISI katika Kaunti ya Kakamega wanachunguza kisa ambapo pasta mwenye umri wa miaka 33 kutoka eneobunge la Bumula anadaiwa kumtapeli mmishenari kutoka Japan Sh1.2 milioni.
Imesemekana sehemu ya fedha hizo zilistahili kutumiwa kuandaa mhadhara wa kuhubiri injili ilhali hilo halikufanyika.
Pasta Benjamin Oruko kutoka kanisa la Word of Deliverance International, alikamatwa Jumapili mjini Bungoma baada ya mmishenari huyo kuwasilisha ripoti kwa afisi za Idara ya Upelelezi wa Jinai Bungoma.
Raia huyo wa kigeni aliyetambuliwa kama Bi Mimi Hagiwara kutoka Japan, anadai alikutana na mhubiri huyo kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook miaka miwili iliyopita akaanza kumtumia fedha kusaidia wenye mahitaji katika jamii.
Akizungumza na wanahabari nje ya afisi za DCI Bungoma, Bi Hagiwara alisema Bw Oruko alimdanganya kwamba alitumia pesa hizo kujenga makao ya watoto mayatima na miradi mbalimbali kama vile ufugaji wa kuku, ng’ombe wa maziwa na kufungua maduka.
Lakini Bw Oruko alipoachiliwa Jumatano jioni kwa bondi, alijitetea kwamba mmishenari huyo alimtumia Sh70,000 pekee ili kuwatafutia makazi na mahitaji mengine walipokuwa wakipanga kuzuru Kenya.
Ilidaiwa pia mhubiri huyo alimdanganya kuwa anapanga kuandaa mhadhara wa mahubiri kuanzia Novemba 24 hadi 27 mjini Bungoma na alimwalika mhubiri aliyemtambulisha kama Pasta Shahzad, mtendaji miujiza kutoka Pakistan ambaye angekuwa mhubiri mkuu.
“Tulipanga kuwa na mhadhara mkubwa mjini Bungoma ambao ungevutia zaidi ya watu 5,000. Tulikuwa hata tumelipa Sh80,000 kwa mkutano huo kupeperushwa moja kwa moja kwenye televisheni kwa sababu alikuwa ameomba fedha hizo ambazo pia zilistahili kutumiwa kwa matangazo,” akasema Bi Hagiwara.
Kulingana naye, alipofika Kenya ndipo aligundua hapakuwa na mpango wowote kama huo kwani hapakuwa hata na mabango yenye picha za Pasta Shahzad kutangaza mkutano huo, jinsi huwa ilivyo kwa kawaida mkutano kama huo unapoandaliwa kokote.
Alizidi kusema walishtuka kupata kuwa Bw Oruko alikuwa amejenga kibanda kidogo ambacho alidai ndicho kanisa.
“Kila wakati tulipomuuliza Oruko picha za miradi tuliyofadhili, alituambia tuwe na subira na angezituma baadaye. Siku moja alitutumia picha za wanawake wakiwa wamebeba kuku,” akaeleza Bi Hagiwara, ambaye aliongeza kuwa Bw Oruko alikuwa ameahidi kuwapeleka kwa viongozi wakuu akiwemo Rais Uhuru Kenyatta na Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati, lakini walipowasili walipelekwa kwa Kamishna wa Kaunti James Kianda ambaye aliwakaribisha rasmi katika kaunti hiyo.