• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Pasta atorokea kisiwani akidai Huduma Namba ni ya kishetani

Pasta atorokea kisiwani akidai Huduma Namba ni ya kishetani

Na GAITANO PESSA

MHUBIRI kutoka kijiji cha Mubwayo, eneo la Bunyala, Kaunti ya Busia ameshangaza wakazi baada ya kuuza mali yake na kuhama, ili kuepuka kujisajili kwa mpango wa ‘Huduma Namba’.

Pasta Peter Lungekhe aidha amekuwa akirai waumini wa kanisa lake kuhama pamoja naye kuelekea kisiwa cha Bulindi, Yala ambapo anasema hakuna atakayewafikia.

Bw Lungekhe anaripotiwa kuapa kuwa katu hatajisajili kwa mpango huo wa serikali, akisema unaashiria mwisho wa dunia.

“Hata mkinipeleka kwa Rais Uhuru Kenyatta nitamwambia kuwa sitajisajili kwa Huduma Namba. Sitaki kitu chochote kinachohusiana na Huduma Namba. Mimi ni mfuasi sugu wa Biblia ambayo ilitabiri hili kuja nyakati za mwisho,” mhubiri huyo wa SDA akasema.

Tangu kuanzishwa kwa mpango wa Wakenya kujisajili kwa Huduma Namba, pingamizi zimeibuka zoezi hilo likihusishwa na ushetani na katika Kaunti hiyo ya Busia, kikundi cha wafuasi wa pasta Lungekhe pia wameuza mali yao, wakijitayarisha kuondoka nchini.

“Tayari nimeaga familia yangu na kuwaambia kuwa tutaonana tena. Na hata tusipoonana bado ni sawa. Hata Biblia inasema Petero alishtakiwa kwa kuhubiri ukweli na kwa hilo niko tayari,” pasta Lungekhe akasema.

Hatua yake, hata hivyo, imevutia maoni tofauti kutoka kwa wakazi, wengine wao wakisema hali inayoshuhudiwa ni kwa kuwa serikali haikuelimisha umma kabla ya kuanzisha zoezi hilo.

“Tunashuhudia kuchanganyikiwa kwa kuwa serikali haikuelimisha umma ifaavyo. Pia, kuharakisha zoezi hili na hali kuwa vifaa ni vichache kumeharibu mambo,” akasema Xlare Ajiambo.

Lakini wakazi wengine kama Peter Ojanji walisema kuwa viongozi wa kidini ndio wanafaa kuwa mstari wa mbele kurai watu kujisajili, badala ya kuhubiri kinyume.

“Naelewa hata Jaji Mkuu David Maraga ni mfuasi sugu wa SDA lakini hajauza mali yake,” akasema Bw Ojanji. Waziri Msaidizi wa Masuala ya Nje Ababu Namwamba amekashifu wale wanaopinga zoezi hilo la serikali, akiwataja maadui wa maendeleo.

“Sioni mahali kuna ushetani katika zoezi la kawaida la serikali kuorodhesha watu. Tuache mambo yasiyosaidia taifa kusonga mbele,” akasema Bw Namwamba.

Kulingana na Kamishna wa Kaunti ya Busia, angalau watu 283,872 (asilimia 81.3) wamesajiliwa katika mpango huo wa NIIMS, kila siku serikali ikilenga kusajili watu 24,000. “Nina furaha wakazi wa Busia wametii wito na kujitokeza kujisajili. Kaunti imebakisha watu 65,000 kutimiza lengo,” akasema kamishna huyo.

You can share this post!

Mvua itanyesha kote nchini, Idara sasa yasema

Shollei motoni kwa kutopigia debe Ruto

adminleo