Habari Mseto

Pendekezo machifu na wazee wa mitaa wafundishwe jinsi ya kutoa ushauri nasaha

September 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MISHI GONGO

VIONGOZI katika chama cha Maendeleo ya Wanawake katika Kaunti ya Mombasa wameomba machifu wote wapewe mafunzo ya kupeana ushauri nasaha.

Walisema kuwa wakazi hukimbilia machifu kwanza katika kutatuliwa masuala mbalimbali ya kijamii.

Aklizungumza na Taifa Leo mnamo Alhamisi mwanachama wa chama hicho Bi Millicent Odhiambo alisema wakazi wanapofikwa na matatizo hukimbilia katika afisi za machifu kabla kuchukua hatua yoyote.

“Wanandoa wanapokumbwa na migogoro, wanawake wanapokabiliwa na dhuluma za kijinsia au watoto wanaponajisiwa, watu hukimbilia kwa chifu kumueleza kabla ya kuenda kuripoti katika vituo vya polisi hivyo ni muhimu wao kuwa na ujuzi wa kutoa ushauri nasaha,” akasema Bi Odhiambo.

Alisema matatizo kama ya ndoa huhitaji mtu mwenye ujuzi kutatua.

“Machifu wakipewa mafuzo hayo wataweza kutatua masuala mengi katika jamii. Suala la usalama huanza na jamii kuongoka au kuwa na maadili mema,” akasema.

Alieleza kuwa chama chao kiko tayari kufanya kazi na serikali kuhakikisha kuwa machifu wanapokea mafunzo hayo.

“Kuna matatizo mengine ambayo tunaweza kusuluhisha mashinani bila kuhusisha afisi za wakuu,” akasema.

Hoja hiyo iliungwa mkono na wakazi wa Frere Town wakisema baadhi ya machifu wanashindwa kuwatatulia masuala madogomadogo.

Bi Odhiambo ambaye pia anashughulika na masuala ya dhuluma za kijinsia alisema visa vya dhuluma za watoto vimepungua katika eneo hilo.

Aliwaomba wazazi kuwa makini na watoto wao.

Aliongezea kuwa baadhi ya visa vya unajisi wa baadhi ya watoto huwa watendaji ni jamaa zao wa karibu kama kaka, binamu, mjomba, babu na kadhalika.

“Hakikisha kuwa unakuwa macho na unafuatilia mienendo ya mtoto wako kwa karibu. Watu unaowaacha na watoto wako hakikisha kuwa ni waaminifu na wenye nidhamu ya hali ya juu,” akasema.

Mwingine Bi Mary Wambo, kiongozi wa maendeleo ya wanawake eneo la Nyali aliliunga mkono pendekezo hilo akisema kuwa litasaidia pakubwa kutatua mizozo ya kijamii.

Alieleza kuwa wazee wa mitaa na machifu ndio wanaohudumia wananchi mashinani.

Walipendekeza hayo mbele ya mshirikishi wa usalama katika eneo la Pwani Bw John Elungata na kamishna wa Mombasa Bw Gilbert Kitiyo.